Na Ally Mohamed, Zanzibar
LIGI Kuu ya Zanzibar, maarufu Zanzibar Grand Malt Premier
League, imemaliza mzunguko wake wa kwanza jana kwa kushuhudia mechi moja
iliyochezwa Uwanja wa Amaan, ikiwakutanisha Chuoni na Mundu kutoka Kaskazini
mwa kisiwa cha Unguja.
Mechi hiyo imemalizika kwa timu ya Chuoni kuibuka na ushindi
wa mabao 2-1, mabao ya Chuoni yote mawili yakifungwa kipindi cha kwanza kupitia
kwa Shaffii Hassan katika dakika ya 44, bao la pili likifungwa na Ahmed Malik
katika dakika ya 44.
Mundu, ambayo iliteremka daraja, lakini wakainunua Miembeni
United iliyobaki Ligi Kuu, ilipata bao lake pekee kupitia kwa Mfanyeje Mussa,
dakika ya 56.
Ligi hiyo inatarajia kuendelea tena Jumamosi wiki hii kwa
michezo miwili, kisiwani Pemba katika Uwanja wa Gombani, mabingwa watetezi wa
ligi hiyo na wawakilishi wa Zanzibar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Super
Falcon wakikipiga na Duma timu inayomilikiwa na Jeshi la Kujenga Uchumi la
Zanzibar (JKU).
Itakumbukwa kuwa mechi iliyopita Super Falcon walipoteza
baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Chipukizi, huku Duma
wakikubali kipigo kama hicho kutoka kwa wawakilishi wa Zanzibar katika kpmbe la
Shirikisho, Jamhuri.
Kisiwani Unguja katika Uwanja wa Amaan, mabaharia wa KMKM
ambao walipoteza mchezo wao uliopita baada ya kukubali kipigo chembamba cha bao
1-0 kutoka kwa Mafunzo, watateremka uwanjani hapo kukabiliana na Malindi ambao
nao katika mechi yao ya kwanza walipoteza dhidi ya Bandari baada ya kukubali
kipigo cha mabao 3-2.



.png)
0 comments:
Post a Comment