• HABARI MPYA

    Thursday, September 27, 2012

    MATAWI YANGA YAKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA KUUA MNYAMA

    Mmoja wa viongozi wa Matawi ya Yanga, Said Motisha akizungumza kwenye Mkutano huo leo


    Wanachama wakipongezana baada ya Mkutano
    Na Emmanuel Ndege
    KATIKA kuhakikisha mnyama hatoki Oktoba 3, mwaka huu- Matawi ya Yanga yamekutana leo katika kikao maalum kujadili namna ya kuifunga Simba siku hiyo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kikao kilichodumu kwa takriban saa mbili, kilifanyika makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani.
    Ajenda kuu, ilikuwa ni kuua mnyama na watu wakagawana majukumu kwa makubaliano kazi inaanza mara moja.
    Wakati huo huo, kikosi cha Yanga kimeingia kambini leo katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam kujiandaa na mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wao hao wa jadi.
    Awali, Yanga ilipanga kwenda kuweka kambi wilayani Bagamoyo mkoani Pwani jana, lakini maamuzi yamebadilika.
    Wakati Yanga, wanaingia kambini leo Changanyikeni, wapinzani wao wa jadi, Simba SC, tayari wapo visiwani Zainzbar tangu juzi saa 11:00 jioni wakijiandaa na mchezo huo wa kukata na shoka, ambao utarushwa moja kwa moja na Televisheni ya Super Sport, kuanzia saa 1:00 usiku.
    Kabla ya kucheza na Simba, Yanga Jumapili itacheza na African Lyon, Uwanja wa Taifa.
    Mechi hiyo inatarajiwa kuwa kali na ya kusisimua, kwa sababu mara ya mwisho timu hizo zilipokutana, Yanga ilifungwa mabao 5-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kipigo hicho ilidaiwa kilitokana na uongozi dhaifu chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na pia ilikuwa sababu ya kumuondoa madarakani kiongozi huyo na kufanyika uchaguzi mdogo, uliomuweka madarakani Yussuf Manji, Mwenyekiti mpya.
    Tangu wakati wa kampeni, miongoni mwa mambo ambayo wana Yanga wamekuwa wakiomba kutoka kwa Manji ni kulipiwa kisasi cha 5-0, ingawa kwa hali ya sasa ya timu hizo, ubora wao haupishani sana, hakuna hakika kama hilo litawezekana. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MATAWI YANGA YAKUTANA KUPANGA MIKAKATI YA KUUA MNYAMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top