• HABARI MPYA

    Saturday, September 22, 2012

    YANGA YATAJA MABOSI WAPYA, YATAJA SABABU ZA KUMTIMUA MTAKATIFU TOM

    Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga akizungumza na Waandishi asubuhi hii. kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Tito Osoro


    MABOSI WAPYA; Kulia ni Oundo na kushoto Mwalusako
    Na Mahmoud Zubeiry
    KLABU ya Yanga imetangaza rasmi kumfukuza Kocha wake Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet na nafasi yake atakaimu Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro hadi hapo atakapopatikana kocha  mwingine.
    Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga amesema asubuhi hii katika Mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani kwamba, matokeo mabaya ndio yamefanya Saintfiet asitishiwe mkataba.
    Aidha, Sanga alikanusha madai kwamba eti kocha huyo amefukuzwa baada ya kutofautiana na Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
    “Timu ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata, yeye aliwaruhusu wachezaji kwenda kulewa baada ya mechi. Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani.
    Kwa mfano timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
    Timu iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi, tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha mkataba wake,” alisemsa Sanga.   
    Saintfiet ameiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai mwaka huu, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo amefungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
    Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi. 
    Pamoja na kufukuzwa kwa kocha, Yanga imemtangaza rasmi beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Lawrence Mwalusako kukaimu nafasi ya Katibu wa klabu hiyo na Dennis Oundo kuwa kaimu Mkurugenzi wa Fedha na Utawala.
    Hatua hiyo, inafuatia kusimamishwa kazi kwa Sekretarieti nzima ya klabu, akiwemo Katibu Celestine Mwesigwa na Ofisa Habari, Louis Sendeu, kutokana na kile ilichoeleza utendaji usioridhisha.
    Wengine waliokumbwa na panga hilo ni Masoud Saad, aliyekuwa Ofisa Utawala, Philip Chifuka aliyekuwa Mhasibu na Hafidh Saleh aliyekuwa Meneja ambaye anahamishiwa kwenye majukumu mengine.
    Mbali na Mwalusako na Oundo, kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Sekilojo Johnson Chambua anatajwa kupewa nafasi ya Umeneja, wakati nafasi ya Msemaji wa klabu iliyoachwa wazi na Louis Sendeu, inaelezwa atapewa mdogo wa mke wa Ridhiwani Kikwete, aliyehesabu kura za Abdallah Bin Kleb katika uchaguzi mdogo wa klabu, Julai 14. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA YATAJA MABOSI WAPYA, YATAJA SABABU ZA KUMTIMUA MTAKATIFU TOM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top