• HABARI MPYA

    Thursday, September 27, 2012

    NSA JOB ASEMA SAFARI IMEANZA KUELEKEA KIATU CHA DHAHABU

    Nsa Job anayebinuka tik tak mbele ya Juma Nyosso wa Simba wakati akiwa Yanga

    Na Princess Asia
    NSA Job amesema safari ya kukimbilia kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilianza rasmi jana Uwanja wa Mkwakwani, Tanga baada ya kufunga mabao mawili katika ushindi wa 3-2 wa Coastal Union dhidi ya Kagera Sugar.
    “Ndio nimeanza, nataka kuwa mfungaji bora msimu huu, hesabu zimeanza sasa, wapenzi na mashabiki wa Coastal watarajie mabao zaidi,”alisema jana alipozungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Tanga.
    Coastal Union jana ilipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi, kufuatia 3-2 dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba, kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikifungana kwa kila kitu na Azam FC.
    Ushindi huo, ulitokana na mabao ya Daniel Lyanga na Nsa Job mawili, ni wa pili katika mechi nne za Wagosi wa Kaya tangu kuanza kwa Ligi Kuu, unakuja siku moja baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Juma Mgunda.
    Mgunda, alijiuzulu jana akisema ameamua kufanya hivyo mapema, kabla ya mambo hayajaribika, ili mwalimu mpya anayekuja afanye kazi vizuri.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY juzi, Mgunda alisema kwamba anaachia timu baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akiwa ameshinda moja na kutoa sare mbili.
    “Kama utaweza kuona naiacha timu ikiwa kwenye hali nzuri kuliko Yanga, ambao wamefungwa mechi moja, sare moja na kushinda moja, naondoka kwa moyo mkunjufu, sina kinyongo na mtu,”alisema.
    Mgunda alisema hiyo ndio hulka yake tangu anacheza Coastal Union, kuwa na moyo swafi na ataendelea kuwa hivyo. “Mimi ni mpenzi wa Coastal Union, hakuna asiyejua, na kwa manufaa ya timu, naondoka,”alisema.
    Kumekuwa kama kuna kampeni ya kumvuruga Mgunda kazini ambayo imekuwa ikiendeshwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kumzomea kila timu inapocheza, hatimaye ameamua kuwaachia timu.
    Kwa sasa Coastal, imebaki na kocha Msaidizi, Habib Kondo ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Villa Squad ya Kinondoni, iliyoshuka daraja na jana ndio aliiongoza timu hiyo ya Barabara ya 13, katika mechi na Kagera Sugar.
    Mgunda anakuwa kocha wa pili wa Ligi Kuu kuachia timu, baada ya Mbelgiiji, Tom Sainftiet ambaye amefukuzwa Yanga, baada ya kutofautiana na uongozi, akiwa ameiongoza timu kwenye mechi mbili tu za Ligi Kuu, akitoa sare moja na kufungwa moja. Hemed Morocco, kocha wa Mafunzo ya Zanzibar yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa Coastal Union ya Tanga, ili awe kocha mpya wa timu hiyo kufuatia kubwagwa manyanga kwa Mgunda.
    Katika mechi nyingine ya ligi hiyo, Polisi Morogoro imelazimishwa sare na Toto African ya Mwanza kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro jioni hii.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSA JOB ASEMA SAFARI IMEANZA KUELEKEA KIATU CHA DHAHABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top