• HABARI MPYA

    Wednesday, September 12, 2012

    HANS POPPE: MGONGOLWA ANAIPOTOSHA IBARA YA 44.3 KWA MASLAHI YAKE BINAFASI

    Hans Poppe

    Na Mahmoud Zubeiry
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wakili Alex Mgongolwa anaipotosha Ibara ya 44.3, kwa kuielezea nusu nusu katika hukumu ya pingamizi la klabu yao dhidi ya Yanga, kuhusu mchezaji Kevin Yondan.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Hans Poppe ambaye ni Kapteni wa zamani wa jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), alisema kwamba Mgongolwa anapotosha na kwa ujumla Kamati yake imekosea kumuidhinisha beki wao Yondan kuchezea Yanga, kwa kuwa klabu hiyo haikufuata taratibu za kumsajili kulingana na maelekezo ya Ibara hiyo.
    Ibara ya 44.3 kuhusu masharti maalum yanayohusu mikataba kati ya wachezaji wa kulipwa na klabu inasema; Klabu inayotarajia kuingia mkataba na mchezaji wa kulipwa, haina budi kuiarifu klabu yake ya sasa kwa maandishi, kabla ya kufanya makubaliano na mchezaji huyo wa kulipwa. Mchezaji wa kulipwa atakuwa huru tu kuingia mkataba na klabu nyingine, iwapo mkataba wake na klabu yake ya sasa utakuwa umekwisha, au unakwisha ndani ya miezi sita, uvunjwaji wowote wa sheria hii, utastahili vikwazo vinavyofaa.       
    Lakini Hans Poppe amesema kwamba anashangaa sana kuona taarifa ya Mgongolwa inasema kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
    “Si kweli, huyu bwana anapotosha, na mbona hakuinukuu yote Ibara hiyo katika taarifa yake? Sasa hii ndio maana sisi tumesema, tunakutana kupanga tarehe ya Mkutano Mkuu, kuomba Baraka za wanachama tujitoe tu kwenye ligi, kwa sababu hatutendewi haki, haki si sahihi,”alisema Hans Poppe.
    Aidha, Mwenyekiti huyo mpya wa Friends Of Simba (F.O.S.) alisema kwamba Ibara ya 45. 6 pia inakazia Ibara hiyo ya 44.3 na kwamba bado anashangaa kwa nini Mgongolwa, ambaye kitaaluma ni Mwanasheria anapindisha sheria za usajili.   
    Ibara ya 45. 6 kuhusu Usajili na Uhamisho wa Wachezaji, inasema; Mchezaji ambaye ameingia mkataba wa zaidi ya msimu mmoja hatoruhusiwa kujisajili na klabu nyingine, kabla ya klabu ya  yake mpya kuafikiana na klabu yake ya zamani (kanuni ya 44.3)   
    Alisema Yanga walimsainisha Yondan mkataba Mei 12, mwaka huu wakati mkataba wake wa awali na Simba ulikuwa unaisha Mei 30, inamaanisha walianza kuzungumza muda mrefu bila kuiarifu klabu yake ya sasa na wakati huo huo, mchezaji huyo aliongeza mkataba Novemba mwaka jana na Simba.
    "Na kama Yanga wangefuata utaratibu huu wa kuzungumza na klabu yake, wangepewa taarifa kama amekwishasaini mkataba mpya,"aliongeza.
    Mapema wiki hii, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF pamoja na kumuidhinisha Yondan kuchezea Yanga, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na beki huyo na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo.
    “Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
    Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa katika taarifa yake aliyoituma BIN ZUBEIRY.
    Mbali na Mwenyekiti Mgongolwa, Wajumbe wengine wa Kamati hiyo waliohudhuria kikao hicho ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo, ambao mwishowe walipiga kura kuamua beki huyo achezee timu gani msimu ujao na ndipo Yanga ikashinda.
    Hata hivyo, inadaiwa katika upigaji kura, tatu zilimbakisha Yondan Simba na tatu zilimpeleka Yanga, lakini kwa kuwa Mwenyekiti ana nafasi ya kupiga kura ya ziada, iwapo kura zimegongana- na siku hiyo Mgongolwa aliitumia kura yake kumpeleka beki huyo Jangwani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE: MGONGOLWA ANAIPOTOSHA IBARA YA 44.3 KWA MASLAHI YAKE BINAFASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top