• HABARI MPYA

    Monday, September 24, 2012

    TWITE AACHWE AGOMBEE NAMBA NA AKINA YONDAN, CANNAVARO, JOB KULIKO KULAZIMISHWA KUCHEZA

    Mbuyu Twite

    Na Mahmoud Zubeiry
    HAIKUWA mbaya Yanga kumsajili Mbuyu Twite, kwa sababu baada ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan, beki mwingine wa kati waliyekuwa naye ni Ibrahim Job pekee.
    Niliamini kusajiliwa kwa Twite, maana yake Yanga itakuwa na mabeki wawili wa kati uwanjani na wawili benchi, lakini sasa si hivyo.
    Ni kama Yanga imeridhika na uchezaji wa pamoja wa Yondan na Cannavaro, lakini inalazimisha na Twite acheze.
    Mwanzoni, Twite alikuwa anapangwa kama kiungo mkabaji, lakini akashindwa kucheza kwa ubora wa Athumani Iddi ‘Chuji’, hivyo akahamishiwa beki ya pembeni.
    Morogoro dhidi ya Mtibwa alipangwa beki ya kushoto, akawa uchochoro wa Hussein Javu na Jumamosi dhidi ya JKT Ruvu alicheza beki ya kulia- pia sikuridhishwa na uchezaji wake, naamini Juma Abdul, Godfrey Tauta, au Nahodha Nsajigwa Shadrack, yeyote angecheza vema zaidi yake.
    Mechi na JKT Ruvu ilikuwa nyepesi kwa Yanga na timu ilishinda na kwa desturi yetu Watanzania, timu inaposhinda watu hawaangaalii makosa ua mapungufu ya timu.
    Twite ni beki wa kati na naamini anaweza kucheza vizuri nafasi hiyo tu, hizo nyingine analazimishwa kwa sababu ni mchezaji nyota na wenye timu yao hawataki aanzie benchi.
    Lakini wapo watu waliosajiliwa maalum kwa ajili ya nafasi hizo, tena wengi mno. Katika nafasi ambazo Yanga imewekeza vizuri kwenye timu yake, basi ni mabeki wa pembeni.
    Kulia peke yake wapo watatu, Nsajigwa, Abdul na Taita na kushoto pia wapo watatu, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika, sasa kama beki wa kati anapelekwa pembeni, hawa waliosajiliwa kwa ajili ya kucheza nafasi hizo wacheze wapi?
    Hapa sasa unaweza kuona Twite anaivuruga Yanga kwa kulazimishwa kucheza na kitu kingine ambacho sielewi Yanga ni kuwachezesha mbele mabeki wa pembeni, wakati timu ina viungo wengi tu wa pembeni.
    Mara nyingi makocha wengi duniani hutumia mabeki mbele katika kujihami na sana hutokea katika mechi ngumu, kama fainali kocha anajua anakutana na timu yenye kushambulia sana, hivyo anaongeza wakabaji uwanjani.
    Lakini kwa Yanga, sasa imekuwa desturi tangu wakati wa Sam Timbe, hata Tom Saintfiet, ingawa juzi Kaimu Kocha Mkuu, Freddy Felix Minziro alibadilisha mfumo huo na tuliona kasi ya mashambulizi Yanga iliongezeka na ikapata ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya JKT Ruvu.  
    Lakini kwa nini Minziro alimpanga Twite beki ya kulia, wakati Nsajigwa, Taita na Juma Abdul wapo na hawakuwa wagonjwa?
    Hakuna sababu ya Yanga kulazimisha kumchezesha Twite, waachwe mabeki wote wanne wa kati, wapiganie namba mazoezini ili pia na kujenga nidhamu ya uwajibikaji, au labda tuambiwe naye amesaini mkataba kama alisoaini Juma Kasaeja na Yanga mwaka 2009, lazima acheze.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TWITE AACHWE AGOMBEE NAMBA NA AKINA YONDAN, CANNAVARO, JOB KULIKO KULAZIMISHWA KUCHEZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top