• HABARI MPYA

    Sunday, September 23, 2012

    MNYAMA SIMBA SC MAWINDONI LEO


    Simba SC
    Na Mahmoud Zubeiry
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuendelea leo kwa mechi tatu kupigwa kwenye viwanja tofauti, macho na masikio ya wengi yakielekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako mabingwa watetezi, Simba SC watakuwa wakimenyana na Ruvu Shooting ya Pwani.
    Simba imeshinda mechi zake zote mbili za awali, dhidi ya African Lyon mabao 3-0 na JKT Ruvu 2-0 na inahitaji ushindi katika mchezo wa leo, ili kurudi kileleni, baada ya Azam jana kuifunga Mtibwa Sugar na kuukamata usukani wa ligi.
    Simba leo itamkosa mshambuliaji wake hatari, Mganda Emanuel Arnold Okwi lakini kocha Mserbia, Milovan Cirkovick anatarajiwa kumrudisha uwanjani mshambuliaji Mzambia, Felix Mumba Sunzu.
    Bado safu ya ushambuliaji ya Simba ina wakali wengine kama Mghana, Daniel Akuffo na mzalendo Mrisho Ngassa, ambao wakiongozwa na viungo mahiri kama Haruna Moshi ‘Boban’ na Mwinyi Kazimoto, moto unatarajiwa kuwa ule ule.   
    Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya Mgambo JKT na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na African Lyon na Prisons kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mechi za jana, Yanga ilipata ushindi wa kwanza ndani ya mechi tatu za ligi hiyo, baada ya kuifunga JKT Ruvu mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hadi mapumziko Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Nahodha, Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ dakika ya nne na Didier Kavumbangu dakika ya 31, mabao yote yakitokana na kazi nzuri ya kiungo mshambuliaji Simon Msuva.
    Bao la kwanza ulikuwa mpira wa adhabu uliopigwa na Haruna Niyonzima, baada ya Msuva kuangushwa karibu kabisa na eneo la hatari la JKT Ruvu na bao la pili dogo huyo aliyesajiliwa kutoka Moro United iliyoshuka daraja, alimpa pasi mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kavumbangu.
    Kipindi cha pili, Yanga walirudi tena kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 52, mfungaji Simon Msuva kabla ya Didier Kavumbangu kufunga la nne dakika ya 65.
    JKT ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 68 mfungaji Credo Mwaipopo.
    Katika mchezo wa leo, Yanga ilicheza vizuri, wachezaji wakionana kwa pasi nzuri ndefu na fupi, tofauti na ilivyokuwa kwenye iliyopita mjini Morogoro, ambako walifungwa 3-0 na Mtibwa Sugar.
    Ikumbukwe mechi ya kwanza, Yanga ililazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons mjini Mbeya.
    Yanga jana ilicheza chini ya kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro, baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet kusitishiwa mkataba juzi usiku, kufuatia kutofautiana na uongozi.
    Kwenye Uwanja wa Chamazi, wenyeji Azam FC waliifunga Mtibwa Sugar 1-0, bao pekee la Kipre Herman Tchetche, wakati Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha wenyeji JKT Oljoro 1-0 wameifunga Polisi Morogoro, bao pekee la Paul Ndonga dakika ya 13 na  Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wenyeji Coastal Union wamelazimishwa sare ya bila kufungana na Toto Africans.

    MSIMAMO WA LIGI KUU BARA

                                 P    W  D   L    GF       GA      GD    P
    Azam FC               3    2    1    -     3          1          2       7
    Simba SC              2    2    -     -     5          -           5       6
    Coastal                  3    1    2    -     2          1          1       5
    JKT Oljoro              3    1    2    1    2          1          1       5
    Mtibwa Sugar         3    1    1    1    3          1          2       4
    Yanga SC              3    1    1    1    4          4          -        4
    Ruvu Shooting       2    1    -     1    3          3          -        3
    JKT Ruvu               3    1    -     2    3          7          -4     3
    African Lyon           2    1    -     1    1          3          -2     3
    Toto African            3    -     3    1    3          2          1       3
    Prisons                   2    -     2    -     1          1          -        2
    Polisi Moro              3    -     1    2    -           2          -2     1
    Kagera Sugar         2    -     1    1    -           1          -1     1
    JKT Mgambo          2    -     -     2    1          3          -2     0
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MNYAMA SIMBA SC MAWINDONI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top