Akuffo ataendelea kuwainua vitini mashabiki wa Simba leo? |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya soka
ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo, timu zote 14 zikijitupa
uwanjani kwa mara ya pili, macho na masikio ya wengi yakielekezwa katika
viwanja vya CCM Kirumba mjini Mwanza, Jamhuri mjini Morogoro na Taifa mjini Dar
es Salaam.
Wakati mabingwa
watetezi, Simba SC wakiwa wageni wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, Mtibwa Sugar watakuwa wenyeji wa Yanga kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini
Morogoro na Mwanza, Toto wataikaribisha Azam FC.
Viingilio
kwa mechi ya Uwanja wa Taifa vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh.
20,000 wakati kwenye Uwanja wa Jamhuri itakuwa sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Mechi
nyingine za ligi hiyo zitakazochezwa leo ni African Lyon vs Polisi Morogoro
kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam. Nayo Ruvu Shooting itashuka
kwenye Uwanja wake wa Mabatini, Mlandizi kuikabili Mgambo Shooting kutoka
Handeni mkoani Tanga.
Tanzania
Prisons itakuwa kwenye Uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya
kuisubiri Coastal Union ya Tanga wakati Oljoro JKT itaitembelea Kagera Sugar
kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kocha Mkuu
wa Yanga SC, Mbelgiji Tom Saintefiet amebeba wachezaji 18 kwa mchezo wa leo na
Mtibwa Sugar, kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ambao ni makipa; Yaw Berko,
Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Shadrack Nsajigwa, Juma Abdul, Godfrey Taita,
Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, David Luhende, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika.
Aliwataja
viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Nizar khalfan,
Shamte Ally na Simon Msuva, wakati washambuliaji ni Didier Kavumbangu, Said
Bahanuzi na Hamisi Kiiza, wakati waliobaki Dar es Salaam ni kipa Said Mohamed,
mabeki Ladislaus Mbogo, Job Ibrahim, viungo Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’,
Salum Telela, Omega Seme, Nurdin Bakari, Idrisa Assega, Issa Ngao wa Yanga B
anayekomazwa kikosi cha kwanza na mshambuliaji Jerry Tegete.
Huo utakuwa
mchezo wa pili kwa Yanga katika ligi hiyo, baada ya awali kulazimishwa sare ya
bila kufungana na Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Jumamosi.
Saintfiet juzi
aliwaomba radhi mashabiki wa Yanga kwa sare ya Jumamosi kwenye Uwanja wa
Sokoine na akawatupia lawama viongozi wa klabu hiyo, kwa maandalizi mabovu.
Saintfiet alilalamikia
kulala kwenye hoteli mbaya, yenye vitanda vichache na vidogo, vilivyosababisha
watu wakalala mzungu wa nne, na chakula kibaya na kwa ujumla alisema hawakuwa
vizuri kabla ya mechi hiyo. Alisema yeye
alilala kitanda kimoja na Louis Sendeu na Mbuyu Twite alibanana na Didier
Kavumbangu na hoteli haikuwa na mabomba vyooni wala bafuni, hivyo kulazimika
kuingia na ndoo na kuogea kata.
Alisema pia
hoteli hiyo ilikuwa katikati ya mji na karibu na stendi ya mabasi, kila
alfajiri kelele nyingi na kwa ujumla timu iliingia uwanjani ikiwa haiku vizuri.
“Mimi kwa
mfano sijaoga siku mbili, kwa kweli tulikuwa katika mazingira magumu na
wapinzani wetu walicheza soka ya kuudhi tangu mwanzo, kupoteza muda, na marefa
hawakuchukua hatua, tulipoteza nafasi kupitia kwa Kiiza (Hamisi) na Msuva
(Simon), siwezi kulaumu mchezaji wangu yeyote, lakini hiyo ndiyo hali
halisi,”alisema Saintfiet.
Alisema
anajua hata Uwanja wa huko, Jamhuri si mzuri na mechi itakuwa ngumu kwa sababu
Mtibwa Sugar nao walitoka sare ya bila kufungana na Polisi katika mchezo wao wa
kwanza Jumamosi na anaiheshimu timu hiyo kama moja ya timu tano kubwa Tanzania,
pamoja na Simba, Azam na Coastal Union.
“Lakini
pamoja na kwamba Simba wamependelewa kupangiwa ratiba ya kuanza kucheza
nyumbani mechi tano mfululiuzo, nakuambia Mei mwaka 2013 Yanga ndio itavishwa
taji la ubingwa wa Ligi Kuu, acha wafurahie sasa hivi, watalia mwisho,”alisema
Mtakatifu Tom.
Simba SC juzi
na jana ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kinesi, Manzese eneo la Urafiki, Dar
es Salaam na Felix Sunzu alikuwa kivutio kwenye mazoezi hayo na haitakuwa ajabu
leo kocha Milovan Cirkovick akimchezesha japo kwa kutokea benchi.
Sunzu
alijituma sana mazoezini juzi na jana- ingawa Daniel Akuffo na Abdallah Juma
nao walifanya kazi nzuri ya kumvutia kocha Milo.
Awali, Milo,
alikaririwa na BIN ZUBEIRY akisema kwamba anamuhitaji Sunzu, ambaye ni mchezaji
ghali katika timu yake, lakini anaweza kucheza bila yeye.
Milo alisema
kwamba Sunzu hakumtumia kwenye mechi ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara dhidi ya African Lyon kwa sababu alichelewa kurudi Dar es Salaam kutoka
kwao Zambia. “Ilikuwa kila siku anasema atakuja kesho, kesho, haji,”alisema.
Sunzu
aliyetua Dar es Salaam siku moja kabla ya mechi na Lyon, katika kipindi cha
takriban wiki tatu hakuwa na timu, kwanza akienda kwenye msiba wa dada yake
Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na aliporejea akaomba ruhusu
ya kwenda kwao Zambia.
Alipoulizwa
kama mchezaji huyo anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kuliko wachezaji wote wa
klabu hiyo, dola 3,500 kwa mwezi, zaidi ya Sh. Milioni 5 za Tanzania, ni muhimu
kwa sasa kwenye kikosi chake, Mserbia huyo alisema; “Ndiyo, ni muhimu,
namuhitaji, lakini naweza kucheza bila yeye,”alisema.
Inaonekana
sasa Milo anatiwa jeuri na washambuliaji wake wapya, Mghana Daniel Akuffo,
Abdallah Juma, Salim Kinje, Mrisho Ngassa na wengine ambao yupo nao tangu msimu
uliopita akina Emmanuel Okwi, pamoja na viungo wenye uwezo wa kufunga kama
Mwinyi Kazimoto, Haruna Moshi na wengineo.
Awali ya
hapo, Milo alisema kwa sasa hawatumii mabeki wake wapya, Komabil Keita kutoka
Mali na Paschal Ochieng kutoka Kenya, kwa sababu anataka kwanza waone timu hiyo
inavyocheza wakiwa nje, ili wajifunze.
Profesa huyo
wa Kiserbia alisema kwamba mabeki hao wawili wa kati wanahitaji muda kabla ya
kuanza kucheza kwa mfumo wa Simba, ingawa amewasifia wote ni wazuri.
Alisema
wakati wowote wanaweza kurudi uwanjani, iwe kwa pamoja au kupangwa na wachezaji
wengine na inawezekana hata kwenye mechi ya leo, Jumatano dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Azam FC jana
walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kirumba mjini Mwanza, ili kuuzoea kabla ya
mechi yao na Toto African leo.
Juzi Azam
walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu (TTC), Butimba mjini humo
kujiandaa na mechi hiyo ambayo tayari imekuwa gumzo mjini Mwanza, wakazi wa Jiji
hilo wakiwa na hamu ya kuwaona mastaa wa Azam wanachezaje.
Azam
iliyoanza vema ligi hiyo kwa ushindi wa 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba,
bao pekee la Abdulhalim Humud dhidi ya wenyeji Kagera Sugar, imepania kuondoka
na pointi zote sita katika mechi zake zote mbili za Kanda ya Ziwa.
Toto Africans
itahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili kurejesha imani kwa mashabiki wake
baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na JKT Oljoro, katika mchezo wa ufunguzi
Jumamosi.
Mserbia
anayeinoa Azam, Boris Bunjak ameomba marefa wachezeshe kwa haki, kwani anaamini
vijana wake wanaweza kushinda pale tu sheria 17 zinapotekelezwa uwanjani na si
vinginevyo.
Kocha huyo
aliwalalamikiwa marefa waliochezesha mechi yao ya Ngao ya Jamii na Simba kwamba
waliwabeba mno wapinzani wake, hata wakatoka nyuma kwa 2-0 na kushinda 3-2.
Kwa upande
wake, Kocha wa Toto, John Tegete amesema kwamba baada ya kulazimishwa sare na
Oljoro, Jumatano watapigana kufa na kupona ili kushinda mechi ya kwanza ya Ligi
Kuu.
“Sare ya
juzi kwa kweli hatukuitarajia, tulicheza vizuri, tulipata nafasi nyingi
tukapoteza, lakini kwa siku mbili hizi tutafanyia kazi makosa yetu na Jumatano
tunaomba mashabiki waje kwa wingi kushuhudia mabadiliko, tunawaahidi
ushindi,”alisema baba huyo wa mshambuliaji wa Yanga, Jerry Tegete.
MSIMAMO WA LIGI KUU BARA
P W D L GF GA GD P
Simba SC 1 1 - - 3 - 3 3
Azam FC 1 1 - - 1 - 1 3
Coastal 1 1 - - 1 - 1 3
JKT Ruvu 1 1 - - 2 1 1 3
Toto African 1 - 1 1 1 - - 1
JKT Oljoro 1 - 1 1 1 - - 1
Yanga SC 1 - 1 - - - - 1
Prisons 1 - 1 - - - - 1
Polisi Moro 1 - 1 - - - - 1
Mtibwa Sugar 1 - 1 - - - - 1
African Lyon 1 - - 1 - 3 -3 0
Kagera Sugar 1 - - 1 - - - 0
JKT Mgambo 1 - - 1 - 1 -1 0
Ruvu
Shooting 1 - - 1 1 2 -1 0
0 comments:
Post a Comment