• HABARI MPYA

    Wednesday, September 26, 2012

    KOCHA WA TIMU YA TAIFA ZANZIBAR KUMRITHI MGUNDA COASTAL

    Hemed Morocco

    Na Mahmoud Zubeiry
    HEMED Morocco, kocha wa Mafunzo ya Zanzibar na timu ya taifa ya visiwani humo, Zanzibar Heroes yupo kwenye mazungumzo na uongozi wa Coastal Union ya Tanga, ili awe kocha mpya wa timu hiyo kufuatia kubwagwa manyanga kwa Juma Mgunda.
    Habari kutoka ndani ya Coastal, mabingwa wa Ligi Kuu 1988, zimesema kwamba mazungumzo yanaendelea vizuri na watakapofikia makubaliano, watatangaza rasmi.
    Mgunda, alijiuzulu jana akisema ameamua kufanya hivyo mapema, kabla ya mambo hayajaribika, ili mwalimu mpya anayekuja afanye kazi vizuri.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Mgunda alisema kwamba anaachia timu baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, akiwa ameshinda moja na kutoa sare mbili.
    “Kama utaweza kuona naiacha timu ikiwa kwenye hali nzuri kuliko Yanga, ambao wamefungwa mechi moja, sare moja na kushinda moja, naondoka kwa moyo mkunjufu, sina kinyongo na mtu,”alisema.
    Mgunda alisema hiyo ndio hulka yake tangu anacheza Coastal Union, kuwa na moyo swafi na ataendelea kuwa hivyo. “Mimi ni mpenzi wa Coastal Union, hakuna asiyejua, na kwa manufaa ya timu, naondoka,”alisema.
    Kumekuwa kama kuna kampeni ya kumvuruga Mgunda kazini ambayo imekuwa ikiendeshwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa kumzomea kila timu inapocheza, hatimaye ameamua kuwaachia timu.
    Kwa sasa Coastal, imebaki na kocha Msaidizi, Habib Kondo ambaye msimu uliopita alikuwa kocha wa Villa Squad ya Kinondoni, iliyoshuka daraja na jioni hii anaiongoza timu hiyo ya Barabara ya 13, katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar.
    Mgunda anakuwa kocha wa pili wa Ligi Kuu kuachia timu, baada ya Mbelgiiji, Tom Sainftiet ambaye amefukuzwa Yanga, baada ya kutofautiana na uongozi, akiwa ameiongoza timu kwenye mechi mbili tu za Ligi Kuu, akitoa sare moja na kufungwa moja.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA WA TIMU YA TAIFA ZANZIBAR KUMRITHI MGUNDA COASTAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top