MABINGWA watetezi, Yanga SC wamerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars jioni ya leo Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yamefungwa na viungo Mganda, Allan Jolly Okello ‘Star Boy’, mawili dakika ya 14 na 69 na mzawa, Mudathir Yahya Abbas dakika ya 42, la kwanza akifungwa kipa mzawa, Metacha Boniphane Mnata, kabla ya kumpisha Mnigeria, Amas Daniel Obasogie aliyekwenda kufungwa mawili, moja kila kipindi.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 57 na kurejea kileleni mwa Ligi Kuu ikiwazidi pointi mbili watani wao, Simba SC kufuatia timu zote kucheza mechi 24.
Kwa upande wao Singida Black Stars baada ya kupoteza mchezo wa leo wanabaki na pointi zao 38 za mechi 24 pia nafasi ya nne kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja moja kwa moja, wakati nyingine mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment