• HABARI MPYA

    Sunday, January 13, 2013

    MASWALI MATANO MAGUMU KUHUSU YULE CHIZI WA JANA AMAAN

    Binti mikononi mwa Polisi

    KATIKA Fainali ya Kombe la Mapinduzi jana kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar alikatiza binti mmoja wa umri kati ya miaka 14 na 16 uwanjani dakika ya 89, wakati timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1 akiingilia jukwaa la Urusi na kutokea upande wa jukwaa kuu, ambako alipokewa na Polisi na kutolewa nje ya Uwanja.
    Refa Ramadhan Rajab Ibada ‘Kibo’ alijaribu kumsimamisha kumsemesha, lakini hakuzungumza chochote na aliendelea kukatiza Uwanja hadi nje ambako alipokewa na askari Polisi na kutolewa nje kabisa ya Uwanja. Mtangazaji wa Uwanja wa Amaan, Farouk Karim aliwatuliza mashabiki akisema binti huyo ametoroka hospitali ya vichaa, Kidongo Chekundu na tayari Polisi wamemkamata na kumrejesha huko.
    Hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30, ambako Gaudence Exavery Mwaikimba aliipatia Azam bao la ushindi dakika ya pili tu tangu kuanza kwa muda wa nyongeza.
    Baada ya tukio hilo, na kudaiwa binti huyo alikuwa chizi na alitoroka hospitali kuna maswali matano ya kujiuliza kulingana na jinsi alivyotambulishwa.
    Tazama jinsi alivyoshikwa mikono kwa nguvu naye ameshika vitu vyake kwa nguvu kulia


    1.          Farouk Karim alisema binti ni chizi alitoroka hospitali ya vichaa, alijuaje na sisi tuliokuwa tunapiga picha uwanjani tulimfuatilia binti huyo hadi anatolewa nje ya Uwanja hakuzungumza chochote mbele ya askari ambao walijaribu kumuhoji na wakati huo huo ndipo MC huyo akatoa tangazo hilo?
    2.          Binti alitambulishwa chizi aliyetoroka hospitali, aliingiaje uwanjani na aliruhusiwa vipi na kali zaidi alitokea sehemu ambayo timu hutokea kuingia uwanjani (Dressing rooms)- huko kuna ulinzi mkali na walinzi huhakikisha yeyote asiyehusika hata Mwandishi wa Habari haingii huko?
    3.          Alikuwa mwenye kujiamini kupita kiasi na alitaka kupita njia alizotaka yeye, kwa mfano Polisi walitaka kumpandisha jukwaani, ila yeye akaendelea kuongoza mbele hadi kwenye geti ambalo walimtolea, kwa nini Polisi walimtii namna ile?
    4.          Kuna vitu alikuwa amevishika mkononi wakati anatakiza Uwanja na aliendelea kuvishika kwa umakini hadi alipotiwa nguvuni na Polisi na kwa nini askari hawakutaka kujua ameshika nini, labda alikuwa amebeba kitu cha hatari mfano wa bomu. Haikutokea hatari hiyo, lakini kwa nini ilichukuliwa kwa urahisi tu?
    5.          Kwa nini alitokea uwanjani wakati ambao refa na wachezaji wa timu zote wapo kwenye lango la timu moja, (la Tusker) wakisubiri kupigwa mpira wa kona- na alipita upande wa katikati ya mstari wa kuugawa Uwanja, jambo ambalo lilimsaidia kukatiza bila kukumbana na kashikashi za mchezo hadi refa aliposhituka kutokana na kelele za mashabiki ndipo akamfuata?    

    Refa akimzuia binti

    Binti anakatiza tu, refa kama anambembeleza hivi

    Binti kwa kujiamini kabisa anakatiza Uwanja
    HITIMISHO;
    Lengo la makala hii, ni kupingana na desturi ya kuchukulia mambo kirahisi kutokana na hisia au dhana, kwani wakati mwingine inaweza kutokea hatari kubwa. Tumeshuhudia nchi hii watu wakijifanya machizi kakini katika hadhara, lakini mwisho wa siku wanafanya mambo ya hatari, mfano kupigwa kiatu kwa rais Mstaafu Alhaj Ally Hassan Mwinyi au namna Ubalozi wa Marekani ulivyolipuliwa nchini mwaka 1998, lazima kuna aina fulani ya uzembe au kuchukulia mambo kirahisi ulifanyika.
    Wale watu wa Uamsho tunajua jitihada zao ziliishia wapi, au ilichukuliwa kama tukio la kishirikina tu kama lile la paka kukatiza uwanjani hapo mwaka 1992 wakati wa mechi ya Simba na Yanga tu, watu wakaamua kutuliza mashabiki kwa kusema ni chizi? Nawasilisha. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MASWALI MATANO MAGUMU KUHUSU YULE CHIZI WA JANA AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top