![]() |
| Gaudence Exavery Mwaikimba akifunga bao jana Amaan |
Na Mahmoud Zubeiry,
Zanzibar
AZAM jana
imetetea Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-1
ndani ya dakika 120 kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar, bao lao la ushindi
likifungwa na Gaudence Exavery Mwaikimba. Je, wajua mabao 10 ambayo amefunga
mshambuliaji huyo na hatayasahau daima maishani mwake? Endelea.
10. Ilikuwa
ni katika fainali ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2013 kwenye Uwanja wa Amaan
Zanzibar, wakati Gaudence alipopokea pasi ya Brian Umony na kuwahadaa mabeki wa
Tusker FC ya Kenya, kabla ya kufumua shuti kali lililotinga nyavuni. Anasema
hatalisahau bao hili kwa sababu liliipa timu yake, Azam FC Kombe la Mapinduzi
naye akitoka uwanjani kama shujaa wa mchezo.
9. Ilikuwa
ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2005, akichezea timu ya mkoa wa
Mbeya, wakati alipowazidi nguvu na maarifa mabeki wa Mtwara kwenye Uwanja wa
Uhuru, Dar es Salaam na kuifungia Mbeya bao la pili na la ushindi ndani ya
dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1. Anasema
hatalisahau bao hili, kwa sababu liliipa Kombe Mbeya na kumjengea yeye heshima
nyumbani, kama mmoja wa wanasoka wakubwa waliowahi kutokea Mbeya.
8. Ilikuwa
ni katika fainali ya Kombe la Taifa mwaka 2011 dhidi ya Mwanza, kwenye Uwanja
wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha alipoifungia Mbeya bao pekee la ushindi
dakika za majeruhi baada ya kutimu dakika 90 za kawaida za mchezo. Anasema
hawezi kulisahau bao hilo, kwa sababu lilimuwezesha pia kuibuka mfungaji bora
wa mashindano hayo na kuzidi kujijengea heshima Mbeya.
7. Ilikuwa
ni katika Ligi Kuu ya Bara mwaka 2005 akiichezea Ashanti United ya Ilala, Dar
es Salaam alipoinusuru kuzama mbele ya Yanga kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
mjini Arusha baada ya kuifungia bao la kusawazisha na kuwakatili Watoto wa
Jangwani kuondoka na pointi tatu. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu ni
kama lilimfungulia njia ya kusajiliwa Yanga, kwani tangu siku hiyo ndipo
viongozi wa timu hiyo walipoanza kuzungumza naye, hatimaye wakamsajili 2006.
6. Ilikuwa
ni mwaka 2007 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa, kati ya Tanzania, Taifa
Stars chini ya kocha Mbrazil, Marcio Maximo alipoifungia bao Stars lililoelekea
kuwa la ushindi dhidi ya Angola Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kabla ya
mshambuliaji wa zamani wa Manchester United ya England, Manucho kuisawazishia
Angola. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu lilimjengea heshima katika
medani ya kimataifa, kwa sababu Angola wakati huo ilikuwa imetoka kucheza Kombe
la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani.
5. Ilikuwa
ni mwaka 2006 kwenye michuano ya Kombe la Tusker, wakati Gaudence Mwaikimba
alipovunja mtego wa kuotea wa mabeki wa Moro United na kumtungua kipa Amani
Simba, kuifungia Yanga bao la pili akitoka kufunga pia la kwanza. Anasema
analikumbuka bao la pili kwa sababu, baada ya kufunga Moro United waligomea
mechi na mchezo ukaishia hapo, Yanga ikitinga Nusu Fainali.
4. Ilikuwa
ni mwaka 2012 katika siku zake za mwanzoni kabisa Azam, wakati alipoifungia
timu hiyo bao la ushindi kwenye Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya
Simba SC Uwanja wa Amaan, Zanzibar katika dakika za mwishoni kabisa za mchezo
wakishinda 2-1. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu liliipeleka Azam
fainali ya michuano hiyo, ambako walifanikiwa kutwaa Kombe la kwanza katika
historia ya timu hiyo.
3. Ilikuwa
ni mwaka 2006 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Rwanda
wakati Gaudence Mwaikimba alipofunga bao pekee la ushindi timu ikiwa chini ya
kocha Dk. Mshindo Msolla. Anasema hawezi kulisahau bao hilo kwa sababu siku
hiyo ndiyo kocha Mbrazil, Marcio Maximo alikuwa amewasili nchini na alikuwa
jukwaani akiangalia wachezaji, hivyo kufanya kwake vizuri kulimfanya aendelee
kuwa timu ya taifa chini ya kocha huyo wa Kibrazil.
2. Ilikuwa
ni mwaka 2007 katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame wakati Mwaikimba alipoifungia Yanga bao la kwanza kati ya mawili ya
kusawazisha, la pili likifungwa na Mkenya Ben Mwalala hivyo kufanya sare ya
2-2. Anasema analikumbuka bao hilo kwa sababu liliirudisha timu yao mchezoni
ikitoka nyuma kwa 2-0 na kupata sare ya 2-2 hivyo kuingia Robo Fainali ya
michuano hiyo mjini Kigali, Rwanda.
1.ilikuwa ni
mwaka 2006 katika msimu wake wa kwanza kwenye klabu ya Yanga, Mwaikimba
alipoifungia Yanga bao la tatu, baada ya kufunga mawili ya awali pia katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Bara dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru, Dar es
Salaam. Anasema hatalisahau bao hilo kwa sababu lilikamilisha hat-trick yake
pekee katika Ligi Kuu kihistoria hadi sasa na kufanya mashabiki warejee makwao
siku hiyo wakiimba jina lake.
Naam, hayo
ndio mabao 10 ambayo Gauedence anasema ataendelea kuyakumbuka daima kati ya
mabao aliyowahi kufunga.
![]() |
| Mwaikimba, akishangilia moja ya mabao aliyofunga |
WASIFU WAKE:
JINA: Gaudence Exavery Mwaikimba
KUZALIWA: Oktoba 5, 1984
ALIPOZALIWA: Kyela, Mbeya
KLABU YAKE: Azam FC
KUJIUNGA: 2012
KLABU ZA AWALI:
Mwaka Klabu
2003-2004: Tukuyu Stars
2004- 2005: Kahama United
2005- 2006: Ashanti United
2006- 2009: Yanga SC
2009-2010: Sur (Oman)
2010: Prisons FC
2011- 2012: Kagera Sugar
2012: Moro United
2012 hadi
sasa Azam FC
![]() |
| Mwaikimba akifurahia na mashabiki wake Kombe la Mapinduzi jana |





.png)