• HABARI MPYA

    Saturday, January 12, 2013

    BINTI AKATIZA UWANJANI, AZAM YATWAA KOMBE LA MAPINDUZI

    Shujaa Mwaikimba baada ya kufunga
    bao la ushindi usiku huu

    Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
    AZAM FC wamefanikiwa kutetea Kombe la Mapinduzi usiku huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar baada ya kuifunga Tusker FC ya Kenya mabao 2-1.
    Kwa ushindi huo, Azam wamezawadiwa Sh. Milioni 10, wakati washindi wa pili Tusker wamepata Sh. Milioni 5.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ramadhan Rajab Ibada ‘Kibo’ aliyesaidiwa na Mwanahija Makame Mfumo na Mgaza Kindundi, hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao.
    Azam ndio walioshambulia zaidi katika kipindi hicho, lakini hawakuwa na bahati ya kufunga bao japo moja. Gaudence Mwaikimba alipewa pasi nzuri na Brian Umony dakika ya 44, lakini shuti lake kali lilidakwa na kipa Samuel Odhiambo.
    Kipindi cha pili, Tusker walirudi na moto mkali na kuanza kusukuma mashambulizi mfululizo langoni mwa Azam.
    Hiyo iliwasaidia mabingwa hao wa Kenya kupata bao dakika ya 60, lililofungwa na Jesse Were aliyeunganisha kwa shuti kali la kimo cha mbuzi pasi ya Robert Omunok.
    Refa akijaribu kumzuia binti wakati anakatiza uwanjani
    Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani Azam FC walisawazisha dakika ya 72 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na beki Mkenya, Joackins Atudo baada ya beki wa Tusker, Luke Ochieng kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
    Katika dakika mbili za nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za mchezo huo, alijitokeza binti mwenye umri kati ya 14 na 16 na kukatiza uwanjani akitokea jukwaa la Urusi.
    Refa alijaribu kumsimamisha, lakini aliendelea kukatiza Uwanja hadi nje ambako alipokewa na askari Polisi na kutolewa nje kabisa ya Uwanja. Mtangazaji wa Uwanja wa Amaan, Farouk Karim aliwatuliza mashabiki akisema binti huyo ametoroka hospitali ya vichaa, Kidongo Chekundu na tayari Polisi wamemkamata na kumrejesha huko.
    Hadi dakika 90 zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1 na ndipo zikaongezwa dakika 30.
    Gaudence Exavery Mwaikimba aliipatia Azam bao la ushindi dakika ya pili tu tangu kuanza kwa muda wa nyongeza baada ya kuwazidi nguvu na maarifa mabeki wa Tusker.
    Kikosi cha Azam leo kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samir Hajji Nuhu, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Humphrey Mieno, Khamis Mcha, Gaudence Mwaikimba, Brian Umony/Malika Ndeule dk126 na Uhuru Suleiman/Seif Abdallah dk64.
    Tusker FC; Samuel Odhiambo, Luke Ochieng, Bright Jeremiah, Martin Kizza, Joseph Shikokoti, Frederick Onyango/Mark Ochiambo dk93, Andrew Tolowa/Edwin Ombasa dk 55, Khalid Aucho/Benson Amianda dk 80, Jesse Were/Andrew Sekayambya dk54, Ismail Dunga/Michael Olunga dk52 na Robert Omunok.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BINTI AKATIZA UWANJANI, AZAM YATWAA KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top