Alex Mgongolwa |
Na Prince Akbar
KAMATI ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana
jana, imeitaka klabu ya Simba kuthibitisha madai yake ya kuingia mkataba na Kevin
Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati hiyo, lakini kwa sasa
beki huyo wa kati anaendelea na maisha Yanga.
Kama ilikutana
jana kutwa nzima, ofisi za TFF, Ilala, Dar es Salaam ili kupitia na kutoa
uamuzi na ushauri kwa masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele yake kuhusu
usajili wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania, inayoanza mwishoni mwa wiki
hii.
“Kwa mujibu
wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Kevin Yondan, hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile
Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini mkataba na klabu yao, imetakiwa
kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na baada ya uthibitisho iwasilishe
malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, au
mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa
katika taarifa yake aliyoituma BIN ZUBEIRY leo.
Kuhusu suala
la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni
za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu
zote katika kumsajili Mbuyu Twite, hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema
kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo alichukua dola 32,000 za Simba na
kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku
21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita
kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho chini ya Mwenyekiti Alex
Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani Madega, Ismail Aden Rage, Llyod
Nchunga na Omari Gumbo.
Kuhusu Mussa
Hassan Mgosi ambaye ameombewa usajili Ruvu JKT kutoka DC Motema Pembe ya
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), na Ayoub Hassan Isiko ameombewa usajili
Mtibwa Sugar kutoka Bull FC ya Uganda. Wachezaji hao hawaruhusiwi kuchezea timu
hizo mpaka Hati zao za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) zitakapokuwa zimepatikana.
Kuhusu Toto
Africans kupinga usajili wa Enyinna Darlinton kwa timu ya Kagera Sugar kwa vile
bado ina mkataba wa mchezaji huyo ambao unamalizika mwakani, kwa upande wake
Kagera Sugar ilisema imemsaini mchezaji huyo kwa vile Toto Africans imeshindwa
kumlipa mshahara ambapo kuna makubaliano rasmi kati ya Ariwodo kuwa klabu hiyo
ikishindwa kumlipa mshahara anaruhusiwa kuondoka.
Uamuzi wa
Kamati ni kuwa Ariwodo ni mchezaji halali wa Kagera Sugar kwa vile Toto
Africans ilishindwa kutimiza masharti ya mkataba.
Kuhusu Ramadhan
Chombo ‘Redondo’, ameidhinishwa kuchezea Simba kwa kuzingatia mchezo wa haki na
uungwana (Fair Play) baada ya klabu hiyo na ile ya Azam kufikia makubaliano
kuhusu mchezaji huyo.
Kuhusu David
Luhende, Yanga ilikiri kutolipa ada ya uhamisho ya Sh. Milioni 5 kama
walivyokubaliana na Kagera Sugar. Awali waliipa Kagera Sugar hundi iliyogonga
mwamba benki (bounced cheque). Shauri hilo lilimalizwa kwa Yanga imetakiwa
kulipa fedha hizo ndani ya siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu.
Kuhusu Super
Falcon dhidi ya Edward Christopher kusaini Simba, Simba imepewa siku 21 kuanzia
Septemba 10 mwaka huu iwe imeilipa Super Falcon fedha za matunzo (compensation)
kwa vile ndiyo iliyomlea mchezaji Edward Christopher aliyesajiliwa katika klabu
hiyo.
Kuhusu Toto
Africans dhidi ya Mohamed Soud kusajiliwa Coastal Union, Toto Africans iliweka
pingamizi kwa maelezo kuwa bado ina mkataba na mchezaji huyo. Hivyo kwa msingi
wa Fair Play, mchezaji huyo ameidhinishwa Coastal Union baada ya makubaliono
kati ya klabu.
Kuhusu Rollingstone
dhidi ya Kigi Makassy kusajiliwa Simba, Simba imetakiwa kuilipa Rollingstone
gharama za matunzo ilizoingia wakati ikiwa na mchezaji huyo kwa kuzingatia
kanuni za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kuhusu Super
Falcon dhidi ya Sultan Juma Shija kusajiliwa Coastal Union, uamuzi wa Kamati ni
kuwa Shija atachezea Coastal Union, na kwa vile yuko chini ya umri wa miaka 23,
Coastal Union itailipa Super Falcon fidia ya fedha ilizotumia kumhudumia
mchezaji huyo.
Kuhusu African
Lyon dhidi ya Razak Khalfan kusaini Coastal, Lyon imesema bado ina mkataba na
mchezaji huyo. Kamati imebaini kuwa mkataba wa mchezaji huyo na Lyon
umemalizika, hivyo ni mchezaji halali wa Coastal Union na kuhusu Flamingo dhidi
ya Kelvin Friday kusajiliwa Azam, Friday ruksa kucheza Azam, lakini klabu hiyo
imepewa siku 21 kuanzia Septemba 10 mwaka huu kuilipa Flamingo gharama za
kuvunja mkataba.
Kuhusu Super
Falcon dhidi ya Robert Joseph Mkhotya kusaini African Lyon, Lyon imeagizwa
kuilipa Super Falcon sh. milioni moja ikiwa ni fidia ya kuvunja mkataba wa
mchezaji huyo ambaye imemsajili.
Fedha hizo
zitalipwa kwa awamu nne kutokana na makato ya mlango yatakayofanywa na TFF.
Falcon itapokea malipo hayo kupitia TFF na kuhusu Oljoro JKT dhidi ya Othman
Hassan kusajiliwa Coastal, Kwa mujibu wa rekodi za TFF, mkataba wa mchezaji
huyo na Oljoro JKT unamalizika mwakani. Hivyo, Othman Hassan ni mchezaji halali
wa Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na klabu hiyo.
Kuhusu Yanga
kupinga Simba kuacha wachezaji wane, Kamati imetupa pingamizi hizo kwa vile
hakuna malalamiko yoyote kutoka kwa wachezaji juu ya kuvunjiwa mikataba yao.
Wachezaji hao walioachwa na Simba ni Danny Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu
Mbiavanga na Lino Masombo.
“Ikiwa
wachezaji hao watakuwa na malalamiko kuhusu kuvunjiwa mikataba suala hilo
litafikishwa katika Kamati kwa ajili ya kusikilizwa na kutolewa uamuzi,”ilisema
taarifa ya Mgongolwa.
Kamati hiyo
pia ilifanyia kazi suala la mgombea Uenyekiti, Michael Wambura katika Chama cha
Soka Mara (FAM) katika uchaguzi uliofanyika Novemba mwaka jana, ambaye Kamati
ya Uchaguzi ya TFF iliondoa jina lake kwa kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.
Wambura
hakuridhika na uamuzi huo akapeleka shauri lake Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Kamati hiyo katika uamuzi wake ilisema haina mamlaka ya kushughulikia shauri
hilo. Baadaye Wambura alikata rufani katika Kamati ya Rufani ya TFF ambayo
ilimpa haki ya kugombea.
Kutokana na
mkanganyiko huo wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwa na uamuzi wa mwisho katika
masuala ya uchaguzi ya wanachama wa TFF, na uamuzi wa Kamati ya Rufani kuhusu
uchaguzi wa mwanachama wa TFF, Sekretarieti ya TFF iliomba mwongozo wa kisheria
kwa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji.
Kwa vile
Kamati hizo mbili (Uchaguzi na Rufani) haziko katika mtiririko wa moja kwa moja
wa utoaji maamuzi, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji iliishauri
Sekretarieti ya TFF kuliandikia Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) ili kupata muongozo juu ya suala hilo.
Katika
muongozo wake, FIFA ilitoa maoni kuwa kwa mujibu wa Katiba ya TFF chombo cha
mwisho cha rufani katika masuala ya uchaguzi kwa wanachama wa TFF ni Kamati ya
Uchaguzi ya TFF. Hata hivyo, FIFA ilishauri kuwa si vizuri chombo kimoja kikawa
msimamizi wa uchaguzi, na chenyewe tena ndiyo kiwe cha mwisho katika uamuzi
kwenye uchaguzi husika.
Hivyo,
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji imetoa mapendekezo mawili
kwenda Kamati ya Utendaji kwa ajili ya marekebisho ya Katiba ili kiwepo chombo
kingine cha rufani pale mgombea anapopinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Mapendekezo
hayo ni; Iundwe Kamati ambayo itakuwa inasikiliza rufani zote zinazotokana na
uamuzi uliofanywa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF
isiwe chombo cha mwisho cha uamuzi kwa rufani zinazotokana na uchaguzi wa
wanachama wa TFF.
AU. Rufani
zote zinazotokana na uchaguzi wa wanachama wa TFF zisikilizwe na Kamati ya
Rufani ya TFF. Kwa maana hiyo Kamati ya Rufani ya TFF ndiyo kiwe chombo cha
mwisho kwa wasiokubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuwasilisha
malalamiko yao.
0 comments:
Post a Comment