• HABARI MPYA

    Tuesday, September 11, 2012

    MASHINDANO YA NDONDI YA TAIFA YASOGEZWA MBELE

    Suleiman Kidunda, mmoja wa mabondia nyota Tanzania, hapa akiwa rais Jakaya Kikwete, naye anatarajiwa kushiriki mashindano ya taifa

    Na Prince Akbar
    SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania (BFT)limeandaa mashindano ya ngumi ya ubingwa wa Taifa, yatakayofanyika kuanzia Septemba 17 hadi 22, mwaka huu, Uwanja wa ndani wa Taifa, kila siku kuanzia saa 9.00 alasiri.
    Rais wa BFT, Makore Mashaga ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba Awali mashindano hayo yalikuwa yamepangwa kufanyika kuanzia Septemba 15, lakini kutokana na Uwanja wa Ndani wa Taifa kuwa na shughuli nyingine ya kimichezo, Ligi ya mpira wa kikapu, sasa mashindano hayo yataanza kutimua vumbi siku mbili mbele zaidi.
    Amesema lengo la mashindano hayo ni kupata timu ya taifa ya ngumi yenye sura ya kitaifa, itakayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara, ili kuanza maandalizi ya mapema na ya uhakika kwa ajili ya kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola 2014, mashindano ya Afrika 2015, mashindano ya Olimpiki 2016, ubingwa wa dunia na mashindano mengine mbalimbali.
    Amesema hadi sasa, jumla ya mikoa 18 imethibitisha kushiriki mashindano hayo, ambayo ni Temeke, Kinondoni, Ilala, Ngome ya JWTZ, JKT, Magereza, Polisi, Pwani, Morogoro, Mbeya, Ruvuma, Dodoma, Kigoma, Kagera, Tanga, Arusha, Tabora na Mwanza.
    Amesema BFT licha ya kutopata udhamini wa uhakika wa kufanikisha mashindano haya, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali umejipanga vema kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa kiwango cha hali ya juu ili kufikia lengo la kupata timu ya taifa kwa wakati kwa maandalizi ya mapema.
    Amesema jumla ya Sh. Milioni 26 zinahitajika kufanikisha mashindano hayo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MASHINDANO YA NDONDI YA TAIFA YASOGEZWA MBELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top