• HABARI MPYA

    Sunday, July 01, 2012

    KOCHA UGANDA ASEMA YANGA INATISHA KULIKO SIMBA

    Mussa Mudde akipasua ukuta wa Express

    Charles Ayikoh

    Na Prince Akbar
    KOCHA wa klabu bingwa Uganda, Express ‘Red Eagles’, Charles Ayikoh amesema kwamba Yanga ni timu bora na hatari zaidi ya Simba, baada ya kucheza na timu hizo jana na leo, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya mechi ya leo dhidi ya mabingwa wa Tanzania, Simba SC, Uwanja wa Taifa, Ayikoh alisema kwamba kama itatokea mechi ya kuwania Kombe, akiambiwa achague timu ya kucheza nayo, atachagua Simba.
    “Nitachagua Simba kwa sababu najua nitashinda, ila Yanga ni hatari sana, siwezi kuomba kukutana nao,”alisema.
    Akifafanua, Ayikoh alisema Yanga inacheza kwa kushambulia mfululizo na muda wote wanakuja tu kwenye lango lako, wakati Simba wanapiga pasi zaidi na hawana makali katika kushambulia.
    “Leo mabeki wangu walikuwa likizo, hawakuwa na kazi, jana ilikuwa hatari sana kwao, Yanga wanashambulia sana,”alisema leo Ayikoh, baada ya sare ya bila kufungana na Simba SC.
    Express ambayo ilifungwa 2-1 na Yanga jana, awali ilicheza na Simba mjini Shinyanga wakatoka sare ya kufungana bao 1-1.
    Hata hivyo, katika mchezo wa leo, Simba ilicheza bila washambuliaji wake watatu hatari, Mganda Emmanuel Okwi, Mzambia Felix Sunzu na mzalendo Haruna Moshi ‘Boban’.
    Jana Yanga ilichanganya wachezaji wake wote hatari, wapya na wa zamani- labda alikosekana Haruna Niyonzima pekee. Jerry Tegete alicheza pamoja na mshambuliaji mpya Simon Msuva kutoka Moro United, wakati viungo walikuwa Frank Damayo, Said Bahanuzi, Nizar Khalfan na Athumani Iddi ‘Chuji’.
    Simba leo pale mbele alianza Abdallah Juma aliyesajiliwa kutoka Ruvu Shooting, aliyecheza nyuma ya viungo hodari kama Patrick Mbivayanga, Mussa Mudde, Uhuru Suleiman, Christopher Edward na Amri Kiemba.
    Simba na Yanga wapo kwenye maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza Julai 14, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Yanga waliopo Kundi C, watafungua dimba na Athletico ya Burundi Julai 14, wakati Simba waliopo Kundi A wataanza na URA ya Uganda Julai 16.
    Timu nyingine inayoshiriki michuano hiyo ni Azam FC iliyopangwa Kundi B, ambayo itafungua dimba na Mafunzo ya Zanzibar Julai 15, Uwanja wa Chamazi.
    Pamoja na kuwa mabingwa wa Uganda, Express inayoundwa na wachezaji wengi chipukizi, watashiriki mwakani Kombe la Kagame kulingana na kanuni za Shirikisho la Soka Uganda (FUFA) na mwaka huu watashiriki URA, mabingwa wa mwaka jana.     
    Simon Msuva jana akichuana na beki wa Express

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA UGANDA ASEMA YANGA INATISHA KULIKO SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top