• HABARI MPYA

    Wednesday, July 25, 2012

    TAI WADOGO WATUA KUIKABILI NGORONGORO


    Na Prince Akbar
    TIMU ya soka ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria, Flying Eagles inatarajiwa kuwasili nchini leo kuanzia saa 10 jioni kwa ndege ya RwandAir ikiwa na msafara wa watu 30 wakiwemo wachezaji 18, tayari kwa mechi ya kwanza ya Raundi ya Pili ya kuwania kucheza Fainali za Afrika, dhidi ya wenyeji, Ngorongoro Heroes Julai 29 mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
    Mechi hiyo ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za 18 za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 zitakazochezwa mwakani nchini Algeria itachezeshwa na waamuzi kutoka Kenya wakati Kamishna ni Charles Masembe kutoka Uganda.
    Flying Eagles inayofundishwa na kocha John Obuh, jana (Julai 24 mwaka huu) ilicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali. Nigeria ililala bao 1-0.
    Msafara wa timu hiyo unaongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Nigeria (NFF), Chris Green. Baadhi ya wachezaji walioko katika kikosi cha Flying Eagles ni Chidi Osuchukwu, Alhaji Gero, Shehu Abdullahi, Aminu Umar, Aliyu Mohamed, Uche Agbo, Jonah Usman, Harrison Egbune, Hassan Abubakar na Yahya Adamu.
    Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP A itakuwa sh. 10,000.
    Wakati huo huo: TFF imesema kwamba Nusu fainali zote mbili za kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) mwaka 2012 zinachezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
    Azam na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) zitacheza nusu fainali ya kwanza kuanzia saa 8 kamili mchana, na kufuatiwa na nusu fainali ya pili kati ya Yanga na APR ya Rwanda itakayoanza saa 10 kamili jioni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAI WADOGO WATUA KUIKABILI NGORONGORO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top