• HABARI MPYA

    Wednesday, July 25, 2012

    WIKI MBILI ZILIZOPITA SIMBA NOMA, WIKI MBILI BAADAYE SIMBA BOMU, JAMANI!


    Wachezaji wa Simba wakiwa wamemuinua juu Kaseja baada ya fainali ya Kombe la Urafiki wiki mbili zilizopita

    SIMBA SC jana imetolewa katika Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kufungwa na Azam FC mabao 3-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Robo Fainali ya mwisho.
    Na Mahmoud Zubeiry
    Mbaya wa Simba jana alikuwa John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote matatu, wakati bao la kufutia machozi la Simba lilifungwa na Shomary Kapombe.
    Japokuwa Bocco aliondoka na mpira jana, lakini nyota wa mchezo alikuwa Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’, ambaye alitawala sehemu ya kiungo na kuiongoza vema timu yake hata ikapata ushindi huo mnono.
    Maneno mengi yameibuka baada ya matokeo hayo, jambo ambalo ni kawaida kwa timu zetu hapa nchini, dosari na kasoro nyingi huzungumzwa baada ya matokeo mabaya. Leo ndio wanasema timu mbovu na hata kocha Milovan Cirkovick amesema timu yake haikuwa tayari kwa mashindano haya.
    Najaribu kujiuliza, Simba imetolewa na Azam, timu ambayo wiki mbili zilizopita ilikutana nayo kwenye fainali ya Kombe la Urafiki na ikashinda kwa penalti 3-1, baada ya sare ya 2-2.
    Wiki mbili zilizopita, Simba ilikuwa noma, ilikuwa inatisha baada ya kuifunga Azam kwa matuta, lakini wiki mbili baadaye, Simba mbovu. Jamani!
    Umefika wakati sasa tuwe watu wa kujadili zaidi hali halisi, kufanya tathmini ya kina ili kubaini makosa yetu, badala ya kupenda kuzungumza kwa chuki, jazba na mazoea. Nimewasikia wachambuzi fulani wa radio moja nchini wanazungumzia Simba- kwanza huwezi kujua pointi yao ni ipi. Mara kukosekana kwa Emanuel Okwi kumepunguza makali ya Simba, ndiyo manaa hata Felix Sunzu amekuwa hatishi sasa.
    Jamani, hilo ni tatizo lililofanya Simba ipoteze mechi ya jana? Watanzania tunapenda kukurupuka tunapotaka kusajili wachezaji bila kufuatilia rekodi zao na ndiyo maana kuna wakati tunaingia mkenge kwa magarasa.
    Sunzu katika mashindano haya ameonyesha hayuko sawa- amekosa mabao ya wazi yasiyopungua 10. Sasa kwa nini uwadanganye wana Simba kukosekana kwa Okwi kunamfanya hata Sunzu awe butu, wakati anapata nafasi akiwa yeye na kipa anamdakisha, anapiga nje, anaanguka, au mpira unamgonga unaondoka.
    Mimi nawaambia wachambuzi wa kibongo, wakumbuke mashindano haya hata kwa ambao hawaendi mpirani, wanapata fursa ya kuona kupitia Super Sport na Star TV- wamekuwa wakimuona Sunzu akipokea pasi za mwisho kama alizokuwa akipewa na marehemu Patrick Mafisango, akipigiwa krosi kama ambazo alikuwa akipigiwa na Okwi, lakini anaishia ‘kumbwelambwela’.
    Lakini Sunzu tangu atue Simba, lini alikuwa mkali hata akawanyima watu usingizi? Aliwafunga Yanga kwa penalti kwenye mechi ya Ngao mwaka jana na kwenye Ligi Kuu, kiungo Mafisango alikuwa mfungaji bora wa timu kwa mabao 10, sikumbuki yeye kama alifikisha hata matano. 
    Huyu ni mchezaji anayelipwa dola za Kimarekani 3,500, takriban Sh.Milioni 5 kwa mwezi Simba SC na huwezi kupata jibu kwa nini anamzidi maslahi Shomary Kapombe. Simba ilimsajili Sunzu baada ya kutupiwa virago El Hilal kwa sababu alikuwa hafungi mabao.
    Simba ilimsajili Sunzu kwa kukumbuka alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Challenge, au watuambie walimfuatilia wapi maendeleo yake baada ya hapo, ikiwa klabu aliyokuwa anaitumikia iliamua kuachana naye kwa sababu hafungi na sasa tushangae nini hafungi Simba? 
    Kuisaidia Simba ni kuzama ndani na kuangalia matatizo ya msingi ya timu, kwa sababu huwezi kuwaambia watu eti Simba leo mbovu, wakati wiki mbili zilizopita wachambuzi hao hao waliisifia Simba inatisha na Juma Kaseja ni kipa bora na wakaitabiria kufanya vizuri kwenye Kagame.
    Sasa nataka nieleze matatizo ya msingi ya Simba yaliyowagharimu leo.

    BEKI YA KUSHOTO;
    Simba ilifanya kosa kumuacha Juma Jabu bila kusajili beki mwingine mbadala hodari wa kushoto, kwani Paul Ngalema aliyesajiliwa badala yake hajamvutia kocha Milovan na ndiyo maana jana akampanga Shomary Kapombe beki ya kushoto.
    Ikumbukwe Amir Maftah aliumia kidole baada ya mechi na AS Vita na ikaelezwa hatacheza tena mashindano haya.
    Kapombe asili yake ni kiungo na anaweza kuchezesha timu vizuri akicheza kulia na hata katikati, ila amekuwa akitumiwa kama beki wa kulia na kati na anacheza vizuri tu, lakini upande wa kushoto umemshinda.
    Kama utaurejea vizuri mchezo wa jana, mipira mingi Azam walikuwa wanapitishia upande wake.
    Kikosi cha Simba kilichoanza fainali Urafiki; Kutoka kulia Kaseja, Obadia, Kiemba, Nyosso, Abdallah Juma na Sunzu. Walioinama kutoka kulia ni Mussa Mudde, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Salim Kinje na Mwinyi Kazimoto.

    UPANGAJI MBOVU WA KIKOSI:
    Lino Masombo na Juma Nyosso wote ni mabeki wa aina moja na lilikuwa kosa kubwa kuwapanga pamoja na hadi sasa bila shaka tumejiridhisha Simba haina beki wa uhakika wa kati, au kocha anataiwa kuisuka upya safu kwa kutumia wachezaji alionao kikosini ikibidi hata kumrejesha sentahafu Mussa Mudde.
    Sina neno Jonas Mkude, alicheza vizuri katika nafasi ya kiungo mkabaji, pasi zake zilikuwa zinafika na mwanzoni alijitajidi na kupunguza makali ya Kipre Michael Ballou hadi alipoumia na kutoka na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Chombo ‘Redondo’.
    Takriban mechi mbili au tatu, Mussa anamdhihirishia Milovan, kwamba hawezi kucheza kama kiungo wa pembeni, lakini anandelea kumlazimisha na hapo ndipo unapoweza kujiuliza viungo wa pembeni akina Kiggi Makassy, Salim Kinje, Uhuru Suleiman na hata Christopher Edward walisajiliwa wa nini?
    Sunzu, tangu mashindano yanaanza amekuwa akiboronga na bado ameendelea kupewa nafasi kwenye kikosi cha kwanza na Danny Mrwanda yupo tena ni huyu aliyeingia kwenye fainali ya Kombe la Urafiki akaenda kusababisha penalti iliyofungwa na Mwinyi Kazimoto, wakati Simba ikiwa nyuma kwa mabao 2-1.
    Kuna vitu vinaendelea ndani ya Simba kiasi kwamba inakuwa vigumu kuamini kama ni matakwa ya kocha, au kuna nguvu za ziada kutoka kwa wajuaji? Tumeona mara kadhaa Haruna Moshi ‘Boban’ huwa mzuri zaidi anapotokea benchi na tumeona cheche za Abdallah Juma, lakini mambo mbona yanaenda kinyume sasa?
    Suala si kufungwa, bali ni kiwango duni cha timu- kwa sababu kufungwa hata timu bora kama Barcelona hufungwa na timu za kawaida kama Chelsea, bali inashitua kuona wachezaji ambao hawako vizuri wanalazimishwa kucheza.
    Lino Masombo kila mpira anaosha- hadi kuna wakati Boban akamkaripia, jamani Simba hawachezi hivyo, Simba wanamtembeza nyoka chini- soka ya kutungua maembe ina wenyewe hapa na wanafahamika.
    Kote nilipoogelea ni katika kutanua mjadala tu, lakini hoja yangu ya leo ni kwamba; wiki mbili zilizopita Simba ilikuwa inatisha, wiki mbili baadaye Simba mbovu, jamani!
    Simba tishio wiki mbili zilizopita
    SIMBA BOMU; Hiki ndio kikosi cha Simba iliyoitwa mbovu jana, kutoka kulia waliosimama Kaseja, Lino Masombo, Mussa Mudde, Jonas Mkude, Haruna Moshi na Sunzu. Walioinama ni Kapombe, Nyosso, Kazimoto, Haruna Shamte na Uhuru.
    MAFUNDI BENCHI; Kutoka kulia Kiemba, Kinje, Mrwanda, Obadia, Kiggi na Waziri Hamadi. Abdallah Juma, Paul Ngalema hawakuvaa kabisa.


    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WIKI MBILI ZILIZOPITA SIMBA NOMA, WIKI MBILI BAADAYE SIMBA BOMU, JAMANI! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top