• HABARI MPYA

    Wednesday, July 25, 2012

    'FUNDI' ISSA KIHANGE KUZIKWA DODOMA KESHO


    Na Princess Asia
    MWILI wa kiungo wa zamani wa Simba SC, Issa Kihange aliyefariki dunia jana maeneo ya nyumbani kwake, Mbezi Jogoo, Dar es Salaam baada ya kuanguka uwanjani wakati akicheza mechi za maveterani, unatarajiwa kusafirishwa kesho asubuhi kuelekea Dodoma kwa mazishi.
    Kipa aliyecheza pamoja na Kihange Simba 1991 na 1992, Iddi Pazi ‘Father’, ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, mama wa marehemu amewasili leo Dar es Salaam na taratibu za mazishi zinaendelea na imeamuliwa kiungo huyo mchezeshaji wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi mwili wake ukastiriwe Dodoma.
    Vyanzo vilisema jana kwamba, Kihange alianguka wakati akishangilia bao alilofunga mazoezini uwanjani hiyo jana na baada ya hapo, alikimbizwa hospitali ya IMTU, Mbezi Interchick ambako umauti ulimfika.
    Issa Kihange alikuwamo na aling’ara kwenye kikosi cha Simba kilichotwaa taji la pili Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka 1991 mjini Dar es Salaam, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu walipotwaa mwaka 1974 Dar es Salaam.     
    Marehemu Issa alijiunga na Wekundu wa Msimbazi mwishoni mwa mwaka 1990, akitokea CDA ya Dodoma ambako aling’ara katika msimu wa Ligi Daraja la Kwanza (sasa Ligi Kuu) Tanzania Bara mwaka 1990.
    Aliichezea Simba kwa misimu miwili mfululizo na kwa mfanikio, 1991 na 1992 kabla ya kutemwa mwaka 1993 na hakuna uhakika kama aliendelea soka baada ya kuondoka Msimbazi.
    Aliondoka Simba na Medali mbili za Dhahabu za Kombe la Kagame, mbali na ile aliyovalishwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam (sasa Uhuru) 1991, wakiifunga SC Villa ya Uganda kwenye fainali mabao 3-0, pia alivalishwa Medali nyingine mwaka 1992, Uwanja wa Amaan, Zanzibar walipoifunga Yanga kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: 'FUNDI' ISSA KIHANGE KUZIKWA DODOMA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top