• HABARI MPYA

    Sunday, July 31, 2016

    UONGOZI SIMBA WAKUBALI MABADILIKO, AVEVA 'ATOKA KWA MSAADA' UKUMBINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Simba SC, Evans Elieza Aveva leo ameondoka anasindikizwa na 'mabaunsa' ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam baada ya kufunga Mkutano Mkuu wa mwaka wa klabu hiyo.
    Aveva alifunga Mkutano huo majira ya saa 7:15 mchana akiwa amefanikiwa kutuliza jazba za wanachama kwa kusema amekubali mchakato wa mabadiliko ya katiba unaotakiwa na wana Simba wengi.
    Wanachama zaidi ya 700 kwa pamoja leo wameshinikiza mabadiliko wakitaka klabu sasa ianze kuuza hisa, ili kutoa fursa kwa matajiri kuwa na nguvu na ndani ya Simba.
    Mangara (kulia) akisafisha njia ili Rais Aveva apite baada ya mkutano
    Wanachama wa Simba leo walikuwa wanataka mabadiliko tu
    Wajumbe wa Kamati mbalimbali za Simba, kutoka kulia Musley Ruwayh, Ramesh Patel na Salim Abdallah
    Rais Aveva alikubali mabadiliko ndipo akafunga Mkutano leo

    Kwenye mkutano huo ulioanza saa 11:00 asubuhi uliokuwa na agenda 10, ulimalizika kwa wanachama hao kupitisha mfumo mpya wa wanachama kununua hisa ili kujinusuru na hali ya ukata kutokana na kukosa fedha za kujiendesha.
    Rais wa klabu hiyo Evans Aveva akiwa na kamati yake ya utendaji kwa pamoja iliridhia mabadiliko ya mfumo ili kujikwamua na tatizo la fedha linaloikumba klabu hiyo kutokana na kukosa fedha na vitega uchumi vya kujiendesha.
    Akizungumza na kuthibitisha kuridhia kwa mabadiliko hayo, Aveva alisema kuwa wameridhia mabadiliko ila lazima waweke aratibu husika ambazo zitatumika kama muongozo.
    Alisema kuwa wataipa kazi nyingine kamati aliyoipa kazi hiyo ya kuchunguza mfumo huo na watakapomaliza kamati yake ya utendaji itakaa na kupitia suala hilo kabla la kuirudisha kwa wanahama.
    “Tumepitisha mabadiliko lakini ni namna gani tutafanya ni lazima kamati walioleta ripoti hii ikae na baadae kamati yangu ya utendaji ili tukimaliza tuwarudishe kwa wanachama ambao watafanya uamuzi wa mwisho,”alisema
    Alisema mabadiliko hayo ya mfumo lazima yaendane na mabadiliko ya pia ya katiba hivyo lazima wanachama wa klabu hiyo wapitishe.
    “Huu ni mlolongo ila hatua ya kwanza ambayo tumeanza nayo ni kuridhia mabadiliko hivyo baada ya hapo lazima vitu vya kufanyiwa kazi kama mabadiliko ya katiba,”alisema.
    Mwisho wa mkutano, Aveva aliondoka akisindikizwa na mabaunsa kadhaa akiwemo, komandoo maarufu wa klabu hiyo na wa muda mrefu, Mangara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UONGOZI SIMBA WAKUBALI MABADILIKO, AVEVA 'ATOKA KWA MSAADA' UKUMBINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top