![]() |
| Azam FC |
AZAM tayari
iko Bukoba, kwa ajili ya mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Jumamosi
dhidi ya wenyeji Kagera Sugar na mkuu wa msafara huko ni mchezaji wa zamani wa
wenyeji wao, Philipo Alando, ambaye kwa sasa ni mmoja wa viongozi wa klabu hiyo
ya Chamazi.
Alando ambaye
alistaafu soka akiwa na jezi ya Azam miaka miwili iliyopita, amepewa jukumu la
kuhakikisha anaiongoza Azam kubeba pointi sita za mwanzoni za Ligi Kuu katika
mechi mbili za Kanda ya Ziwa, baada ya mechi ya keshokutwa watakwenda Mwanza,
kuivaa Toto African.
Kocha Mkuu
wa Azam FC, Mserbia Boris Bunjak amesema timu yake ipo tayari kwa Ligi Kuu,
lakini tu amehadharisha marefa wachezeshe kwa haki.
Bunjak alikerwa
mno na marefa waliochezesha mechi ya Ngao ya Jamii Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam juzi kwamba waliwabeba wapinzani wao Simba SC.
Mechi hiyo
ilichezeshwa na Martin Sanya, aliyeisaidiwa na Omar Kambangwa na Ephron Ndissa,
wakati refa wa akiba alikuwa Oden Mbaga na Kamisaa Omary Kasinde.
Akizungumza
na BIN
ZUBEIRY baada ya mechi hiyo, Bunjak alisema kwamba marefa hao
walionyesha mapungufu makubwa kwa kuwapendelea wazi wazi Simba na hata wakafanikiwa
kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2.
“Nafikiri
tulicheza mechi nzuri, tukaongoza 2-0, baada ya hapo tukapoteza nafasi nzuri za
kufunga, lakini siamini kwa nini refa alitoa penalti dakika ya mwisho(kipindi
cha kwanza), kwa sababu ule mpira ulikuwa kwenye himaya ya wachezaji watatu
kutoka nyuma, unaweza kuonaje nani aliucheza kwa mkono.
Bao la pili
pia, pia ulikuwa msaada mkubwa, niliandaa timu yangu kucheza dhidi ya wachezaji
10, siyo wachezaji zaidi, mimi si kocha nayeandaa timu kucheza dhidi ya
wachezaji wengi, naweza kufanya nini, tulicheza vizuri, tulipoteza nafasi, refa
alitunyima penalti mbili, asilimia 100, naweza kufanya nini, labda hii ni soka
ya Tanzania tu.
Nitafanya
nini, huu ni uzoefu wangu wa kwanza ofisini tena, lakini nimeshashangazwa sana,
Simba ni timu kubwa, Simba ni timu nzuri, lakini leo Azam imecheza vizuri, Azam
ilistahili kushinda taji,”alisema.
Kocha huyo
alionyeshwa kuridhishwa na bao moja moja tu la Simba, la tatu ambalo alisita kulizungumzia
kabisa katika malalamiko yake.
Azam juzi
iliiruhusu Simba SC kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2, hivyo kutwaa Ngao
ya Jamii, kwa mara ya pili mfululizo Uwanja wa Taifa, Dar e s Salaam.
Shujaa wa
Simba jana alikuwa ni kiungo Mwinyi Kazimoto aliyefunga bao la ushindi dakika
ya 78 kwa shuti kali la mbali baada ya kumchungulia kipa wa Azam, Deo Munishi
‘Dida’ amekaaje.
Hadi
mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na John
Raphael Bocco ‘Adebayor’ na kipre Herman Tchetche, wakimtungua kipa namba moja
Tanzania, Juma Kaseja.
Bocco
alitangulia kufunga dakika ya tano ya mchezo huo, baada ya kupigiwa kona fupi
na Abdi Kassim ‘Babbi’, akatoa pasi kwa Abdulhalim Humud ambaye alimrudishia
mfungaji huyo akafumua shuti kali la chini likajaa nyavuni pembezoni mwa lango
kulia.
Bocco ambaye
alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Simba SC leo, alimtoka Amir Maftah
upande wa kulia wa Uwanja na kuingia ndani kabla ya kutoa krosi fupi kwa Kipre
aliyemtungua Kaseja na kuipatia Azam bao la pili dakika ya 35.
Simba
ilipata bao lake la kwanza dakika ya kwanza ya muda wa nyongeza, baada ya
kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, mfungaji Daniel Akuffo kwa penalti,
baada ya Said Mourad kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Kipindi cha
pili Simba walirudi na nguvu zaidi na kuamua kushambulia kwa mipira ya pembeni,
ikiwatumia Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi ambao walikuwa wakibadilishana
reli.
Kwa staili
hiyo, haikushangaza Simba ilipotumia dakika 45 za mwisho kwa kufunga mabao
mawili yaliyowatoa nyuma kwa 2-1 na kuibuka kidedea kwa ushindi wa 3-2.
Emanuel Okwi
alimchambua kama karanga Erasto Nyoni na kuingia ndani kabisa akiwatoka mabeki
wengine wa Azam, kabla ya kuujaza mpira nyavuni kwa shuti kali na Kazimoto akamaliza
kazi dakika ya 78.
Kwa ujumla
katika mchezo huo, Azam ilitawala kipindi cha kwanza na ilikosa mabao mawili
zaidi ya wazi kupitia kwa Himid Mao na Kipre, lakini kipindi cha pili Simba
walitawala mchezo na kama wangekuwa makini, nao wangeweza kuvuna mabao
zaidi.
Naibu Waziri
wa Kazi, Makongoro Mahanga alimkabidhi ngao Nahodha wa Simba, Juma Kaseja baada
ya mechi hiyo, ambaye alikwenda kushangilia na wachezaji wenzake na mashabiki
wa timu hiyo.



.png)
0 comments:
Post a Comment