• HABARI MPYA

    Saturday, September 01, 2012

    VIWANJA VINNE TU NDIO SAFI KWA LIGI KUU


    Uwanja wa Mkwakwani; Moja ya viwanja vilivyo katka hali mbaya. Hata vyoo ni tatizo
    Na Princess Asia
    WAKATI zimebaki wiki mbili kabla ya kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hali ya viwanja vingi ni mbaya na hakuna jitihada ya kuviboresha kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
    Uchunguzi uliofanywa na BIN ZUBEIRY, umegundua kwamba ni viwanja vinne tu kati ya viwanja 10 vinavyotarajiwa kutumika kwa ajili ya ligi hiyo ndio vipo katika hali nzuri, inayokidhidi vigezo.
    Viwanja hivyo ni Taifa, Dar es Salaam, ambao utatumiwa na klabu za Yanga na Simba, Chamazi wa Azam, ambao unaweza kutumiwa pia na African Lyon na JKT Ruvu, Manungu wa Mtibwa Sugar na CCM Kirumba wa Toto African.
    Viwanja vingine, Mabatini uliopo Chalinze wa Ruvu Shooting, Mkwakwani, Tanga wa Coastal Union na Mgambo Shooting, Jamhuri Morogoro wa Polisi, Kaitaba, Bukoba wa Kagera Sugar, Sheikh Amri Abeid, Arusha wa JKT Oljoro na Sokoine, Mbeya wa Prisons vipo katika hali mbaya.
    Viwanja vingi kati ya hivyo, eneo lake la kuchezea ni gumu, kuna mabonde na hata nyasi zake hazijastawi vizuri, hali ambayo inahatarisha hata maisha ya wachezaji wenyewe kuumia. Hakuna dalili za jitihada haswa aidha za uongozi wa serikali za mikoa au vyama vya soka vya mikoa husika kuboresha viwanja hivyo kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    Ligi Kuu itaanza Septemba 15 mwaka huu, kwa timu zote 14 kujitupa kwenye viwanja tofauti na mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Simba vs African Lyon (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Polisi Morogoro vs Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons vs Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT vs Coastal Union (Mkwakwani, Tanga), JKT Ruvu vs Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), Kagera Sugar vs Azam (Kaitaba, Bukoba) na Toto Africans vs Oljoro JKT (Kirumba, Mwanza).
    Mzunguko wa kwanza (first round) utamalizika Novemba 11 mwaka huu ambapo kwenye mzunguko huo mechi ya watani wa jadi Yanga na Simba itachezwa Oktoba 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ligi hiyo itamalizika Mei 18 mwakani kwa mechi kati ya Toto Africans vs Ruvu Shooting (Kirumba), Mgambo JKT vs African Lyon (Mkwakwani), JKT Ruvu vs Mtibwa Sugar (Azam Complex), Tanzania Prisons vs Kagera Sugar (Sokoine), Simba vs Yanga (Uwanja wa Taifa), Oljoro JKT vs Azam (Sheikh Amri Abeid Kaluta) na Polisi Morogoro vs Coastal Union (Jamhuri).
    Endapo Simba na Azam hazitafanikiwa kuvuka hatua mojawapo ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, ratiba hiyo itafanyiwa marekebisho.
    Wakati huo huo: Mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi rasmi wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 kati ya bingwa mtetezi Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Septemba 11 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIWANJA VINNE TU NDIO SAFI KWA LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top