Roberto Mancini akiwa na winga mpya, Scott Sinclair
Na Neil Custis, Manchester
ROBERTO MANCINI hajaridhishwa na usajili wa pauni Milioni 52 jumla kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
City iliwanasa kwa pauni Milioni 16, Javi Garcia, Milioni 12, Matija Nastasic, Milioni 6, Scott Sinclair na Milioni 3 Maicon jana baada ya awali kumsajili kwa pauni Milioni 15, Jack Rodwell.
Lakini kocha Mancini amesema mabingwa hao wa England walishindwa kumpatia wachezaji chaguo la kwanza aliowataka, wakiwemo Robin van Persie, Eden Hazard, Javi Martinez na Daniele De Rossi.
Mancini alisema: “Nilichanganyikiwa, kwani vigumu kufanya kila kitu katika wiki moja au siku 10. Ukimaliza msimu, unakuwa na kikao na klabu. Unazungumzia kuhusu wachezaji, lakini wakati fulani haiwezekani kuwapata wachezaji wote unaowataka.
“Unaweza kupata chaguo tofauti. Lakini kuwapata wachezaji tuliowanunua, nimefurahi.”
Mancini alitumia muda mwingi wa usajili kulumbana na Ofisa Utawala wa City, Brian Marwood kwa kushindwa kumpatia wachezaji chaguo la kwanza kwenye orodha yake.
Mwishowe, Van Persie wa Arsenal akaenda kwa mahasimu wao, Manchester United kwa dau la pauni Milioni 22, Hazard akajiunga na Chelsea kwa pauni Milioni 32 kutoka Lille, Martinez akakamilisha uhamisho wake wa pauni Milioni 32 kutoka Athletic Bilbao kwenda Bayern Munich na De Rossi akaamua kubaki Roma.
City imempata kiungo mkabaji wa Benfica, Garcia, mwenye umri wa miaka 25, katika saa ya mwisho (saa 5:00 usiku) kuelekea kufungwa kwa dirisha la usajili. Atachukua mikoba ya Nigel de Jong, ambaye amejiunga na AC Milan kwa pauni Milioni 5.
Beki Mserbia, Nastasic, mwenye umri wa miaka 19, ambaye anaitwa ‘New Nemanja Vidic’, ametua kutoka Fiorentina, wakati winga Sinclair, mwenye umri wa miaka 23, amesaini kutoka Swansea na beki wa pembeni wa Kibrazil, Maicon, mwenye umri wa miaka 31, ametua pia kutoka Inter Milan. City pia imempata kipa wa zamani wa England, Richard Wright, mwenye umri wa miaka 34 kama mchezaji huyu.
SOURCE: http://www.thesun.co.uk
0 comments:
Post a Comment