• HABARI MPYA

    Saturday, July 16, 2016

    BASATA YAUFUNGIA ‘PALE KATI PATAMU’ WA NEY WA MITEGO

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    BARAZA la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati patamu’ ulioimbwa na msanii Emmanuel Elibariki 'Ney wa Mitengo' kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili.
    Katibu Mtendaji wa BASATA, Godfrey Mngereza amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo kwamba Ney amekuwa na tabia na mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka maadili. 
    Amesema kazi zake zimekuwa zikikiuka maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.
    BASATA imeufungia wimbo wa Pale Kati Patamu wa Ney wa Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa wa maadili

    "Ieleweke kwamba kwa mujibu wa kifungu namba 4 (L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa,"amesema.
    Aidha, Mngereza amesema BASATA imewahi kumuita na kumuonya Ney mara kadhaa kutokana na tabia yake ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana na tabia hiyo. 
    Amesema kwa Ney kuendelea kwake kufanya matukio hayo kwa makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. 
    Ametolea mfano wimbo mpya wa Ney uitwao Pale Kati Patamu ambao unasambazwa mitandaoni ukipambwa na picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama. 
    Amesema BASATA haitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa na wasanii kuwa genge la wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa jamii na kwamba wanaufungia wimbo huo rasmi kutumika kwa namna yoyote ile. 
    Pamoja na kuufungia, Mngereza amesema hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na amewataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BASATA YAUFUNGIA ‘PALE KATI PATAMU’ WA NEY WA MITEGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top