• HABARI MPYA

    Saturday, September 01, 2012

    YANGA SC NA COASTAL TAIFA LEO BILA INJINI NNE ZA MAANA

    Yanga SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA ya Dar es Salaam leo inashuka kwenye Uwanja wa nyumbani, Taifa kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa kirafiki kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, iliyopangwa kuanza Septemba 15, mwaka huu.
    Beki Kevin Yondan amepona na leo anaweza kuanza na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika safu ya ulinzi, lakini viungo Nizar Khalfan, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’ na Athumani Iddi ‘Chuji’ bado ni wagonjwa tangu timu ilipokuwa Rwanda wiki iliyopita.
    Kocha Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet, raia wa Ubelgiji aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wakati viungo hao wataikosa mechi ya leo, wachezaji wengine watatu, beki Mbuyu Twite, kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Didier Kavumbangu hawana asilimia 100 ya kucheza mechi ya leo.
    Huo utakuwa mchezo wa 11 kwa Yanga chini ya Mtakatifu Tom na katika mechi zote alipoteza moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi kwenye michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambayo waliibuka mabingwa. Mechi za Kagame, Yanga ilifungwa moja na katika mechi za kirafiki haikufungwa hata moja.   
    Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo Julai mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
    Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
    Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
    Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
    Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
    Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
    Kwa upande wa Coastal, huo utakuwa mchezo wa tano wa kujipima nguvu awali ikishinda mechi moja na kufungwa tatu. Tayari umetokea mgawanyiko baina ya viongozi wa Coastal kuhusu benchi la ufundi la klabu hiyo, linaloongozwa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda, akisaidiwa na Habib Kondo, Kocha wa mazoezi ya viungo, Ally Jangalu na Kocha wa makipa, Bakari Shime.
    Baadhi ya viongozi wa Coastal wanaunga mkono, lakini wengine wanapingana na wazo hilo, wakidai bado ni mapema sana na hasa ikizingatiwa timu ipo kwenye mechi za kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hali ilikuwa mbaya zaidi Jumatano wiki hii, baada ya Coastal kufungwa mabao 2-0 na Bandari ya Mombassa, Kenya katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
    Baada ya mchezo huo, mashabiki wa Coastal waliwatia kashikashi makocha Juma Mgunda na Msaidizi wake Habib Kondo wakidai hawafai na kutaka waondolewe, hali ambayo ilifanya waondolewe uwanjani kwa msaada wa Polisi.
    Hali hiyo ilijitokeza kwa mara ya pili, baada ya Jumatatu pia wiki hii timu hiyo ikicheza na JKT Oljoro ya Arusha pamoja na kushinda bao 1-0, mashabiki walilalamikia kiwango kibovu na kuzomea makocha.

    REKODI YA SAINTFIET YANGA
    1.                      Yanga Vs JKT Ruvu 2-0
    2.                      Yanga Vs Atletico (Burundi) 0-2
    3.                      Yanga Vs Waw Salam (Sudan Kusini) 7-1
    4.                      Yanga Vs APR (Rwanda) 2-0
    5.                      Yanga Vs Mafunzo (Z’bar) 1-1 (5-3penalti)
    6.                      Yanga Vs APR (Rwanda) 1-0
    7.                      Yanga Vs Azam 2-0
    8.                      Yanga Vs African Lyon 4-0
    9.                      Yanga Vs Rayon (Rwanda) 2-0
    10.                    Yanga Vs Polisi (Rwanda) 2-1
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC NA COASTAL TAIFA LEO BILA INJINI NNE ZA MAANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top