• HABARI MPYA

    Sunday, September 02, 2018

    UCHAGUZI MKUU SIMBA SC KUFANYIKA NOVEMBA 3 DAR ES SALAAM, FOMU KUANZA KUTOLEWA KESHO MSIMBAZI

    Na Lisa John, DAR ES SALAAM
    UCHAGUZI Mkuu wa klabu ya Simba SC utafanyika Novemba 3 mwaka huu katika ukumbi ambao utatajwa baadaye mjini Dar es Salaam. 
    Taarifa ya Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Boniphace Lihamwike imesema kwamba fomu za kugombea zitaanza kutolewa kesho Jumatatu kuanzia Saa 4:00 makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi. 
    Hiyo ni baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wao.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.

    Wanachama wa Simba SC watachagua viongozi wapya Novemba 3, mwaka huu

    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
    Katiba mpya ya Simba SC inaelekea Rais wa klabu awe na elimu ya kiwango cha Shahada ambaye ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake.
    Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UCHAGUZI MKUU SIMBA SC KUFANYIKA NOVEMBA 3 DAR ES SALAAM, FOMU KUANZA KUTOLEWA KESHO MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top