• HABARI MPYA

  Sunday, September 23, 2018

  VIONGOZI SIMBA SC WANAAMSHA HASIRA ZA MASHABIKI KWA KUTOKUWA WAWAZI KUHUSU MASOUD JUMA

  KATIKA mechi mbili zilizopita za Ligi Kuu za Simba, Kocha Msaidizi Masoud Juma hakusafiri na timu viongozi wakisema alibaki Dar es Salaam kwa shughuli maalum ikiwa ni pamoja na kutazama mechi za wapinzani wao wajao.   
  Pamoja na hayo, imeelezwa Mrundi huyo aliachwa Dar es Salaam timu ikienda kutoa sare ya 0-0 ya Ndanda FC mjini Mtwara na kufungwa 1-0 na Mbao FC ili kuwasimamia wachezaji wachache ambao hawakusafiri na timu, wakiwemo beki Juuko Murshid na kiungo Haruna Niyonzima.
  Lakini, vyombo vya Habari vimekuwa vikiripoti Mrundi huyo ametofautiana na kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J Aussems na ndiyo maana viongozi wameamua kuwatenganisha kwa sasa.

  Baada ya kipigo cha Mbao FC Alhamisi wiki hii, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza mashabiki walimshambulia kwa chupa kocha huyo na wachezaji huku wakipeleka ujumbe wa kutaka Masoud arejeshwe kwenye timu.
  Misukosuko hiyo ikamsukuma Msemaji wa timu, Hajji Manara kutoa taarifa ya klabu ya kutaka kufanya maamuzi magumu kwa maslahi ya klabu, lakini bila presha. 
  “Bodi ya Wakurugenzi, Sekretarieti, Benchi la Ufundi na wachezaji wa klabu ya Simba wanawaomba radhi wanachama na mashabiki wetu kwa matokeo ya leo (jana). Tumeumia sote na tunawaomba mjue hii ni mechi ya nne tu. Tutafanya maamuzi sahihi bila presha kwa maslahi makubwa ya timu na klabu, ninawaomba mtulie katika kipindi hiki," alisema Manara.
  Juma aliwasili nchini Oktoba 19, mwaka mwaka jana akitokea Rwanda alipokuwa anafundisha timu ya Rayon Sport, kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja aliyeng’atuka.
  Alianza kazi chini ya Mcameroon, Joseph Omog lakini akafukuzwa, akaletewa Mfaransa, Pierre Lechantre aliyemalizia msimu na timu ikatwaa ubingwa kabla ya kufukuzwa – na Mbelgiji, Patrick J Aussems anakuwa kocha wa tatu mkuu wa Mrundi huyo.
  Lakini wakati Lechantre anaondoka alimtupia lawama Juma akidai alimsaliti na inaelezwa alitafuta nafasi ya kuzungumza na Aussems kumueleza juu ya kocha huyo wa Burundi. 
  Wakati uongozi wa Simba SC unasubiriwa kutoa hayo maamuzi magumu, huenda yakawa yenye ahueni kwa Juma baada ya vurugu za Mwanza na iwapo matokeo hayatakuwa mazuri na leo pia dhidi ya Mwadui kule Shinyanga.
  Ukirejea namna ambavyo Lechantre aliondoka timu ikiwa kwenye mashindano mjini Nakuru nchini Kenya, unaweza kuona udhaifu unaanzia kwenye uongozi wa Simba SC chini ya Kaimu Rais, Salum Abdallah ‘Try Again’.
  Viongozi wa Simba SC ndiyo mabosi wa hawa makocha wanapaswa kuwa na misimamo na wepesi wa kufanya maamuzi kwa hayo wanayoyaita maslahi ya klabu na si kusubiri hadi yatokee yaliyotokea Kirumba ndipo watoe tamko.
  Kama uongozi wa Simba SC umejiridhisha Masoud ndiyo tatizo uamue juu ya hatma yake ili mashabiki nao wamuondoe kwenye fikra na hisia zao kuliko kuwahadaa watu eti amebaki Dar kwa kazi maalum, wakati kazi mahsusi iliyomleta ni kuwa Mwalimu wa timu kwenye mashindano.
  Simba SC kufungwa au kutoa sare si shida kubwa, tatizo ni mashabiki hawaelewi nini haswa kinaendelea katika timu, kwani Masoud kabaki Dar wakati wanaona mawazo na fikra zake akiwa kwenye benchi vingeweza kuisaidia timu.
  Makocha wengi na wazuri wameondoka Simba SC kuanzia enzi za akina Naby Camara na hawa waliofuatana mfululizo miaka ya karibuni akina Patrick Phiri, Milovan Cirkovic, Patrick Liewig, Zdravko Logarusic, Goran Kopunovic, Dylan Kerr, Omog na Lechantre na mashabiki waliwasahau na kuwapa ushirikiano walimu wapya.
  Hakuna tatizo kwa mashabiki wa Simba SC kumuondoa kwenye fikra zao Masoud iwapo uongozi utakuwa na msimamo na kutoa maamuzi, kuliko kuwahadaa wanachama, wapenzi na mashabiki wa timu eti amebaki Dar es Sakaam kwa kazi maalum. Ipi?
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VIONGOZI SIMBA SC WANAAMSHA HASIRA ZA MASHABIKI KWA KUTOKUWA WAWAZI KUHUSU MASOUD JUMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top