• HABARI MPYA

  Saturday, September 22, 2018

  COASTAL UNION YANG’ARA MLANDIZI, YAIPIGA RUVU 1-0, BIASHARA UNITED HAITISHI NYUMBANI

  Na Sada Salmin, MLANDIZI
  TIMU ya Coastal Union imepata ushindi wa 1-0 ugenini kwa Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika jioni ya leo.
  Ushindi huo umetokana na bao la kujifunga la beki wa zamani wa Coastal Union Tumba Swedi dakika ya 64 akiwa katika harakati za kuokoa.
  Na kwa matokeo hayo Coastal Union inayofundishwa na mchezaji wake wa zamani, Juma Mgunda inafikisha pointi tisa baada ya kucheza mechi sita, wakati Ruvu inabaki na pointi zake mbili baada ya kucheza mechi tano.   
  Mechi nyingine ya leo, Biashara United imelazimishwa sare ya bila kufungana na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Karume Musoma mkoani Mara.

  Hiyo inakuwa sare ya tatu mfululizo katika mechi za nyumbani baada ya kutoka 0-0 pia na Azam FC na 1-1 na Kagera Sugar katika mechi zake mbili zilizopita Uwanja wa Karume.
  Kwa matokeo hayo, BUM inafikisha pointi sita katika mechi ya sita, wakati JKT Tanzania ambayo nayo kama Biashara imepanda Ligi Kuu msimu huu, inafikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi sita. 
  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi nne, Mwadui FC wakiikaribisha Simba SC Saa 10:00 jioni Uwanja wa Mwadui Complex, mkoani Shinyanga, Mbeya City na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Saa 8:00 mchana, Alliance FC na Azam FC Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Yanga SC na Singida United Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: COASTAL UNION YANG’ARA MLANDIZI, YAIPIGA RUVU 1-0, BIASHARA UNITED HAITISHI NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top