• HABARI MPYA

  Friday, September 28, 2018

  NGOMA AANZA KAZI AZAM FC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA LIPULI CHAMAZI

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC imelazimishwa sare ya bila kufungana na Lipuli FC ya Iringa katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaifanya Azam FC ijiongezee pointi moja na kufikisha 12 baada ya kucheza mechi sita, wakati Lipuli FC ya kocha Suleiman Matola inafikisha pointi nane tu katika mechi ya sita.
  Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm leo alimchezesha mshambuliaji wake Mzimbabwe, Donald Ngoma kwa mara ya kwanza katika mechi ya Ligi Kuu tangu asajiliwe kutoka Yanga, lakini akashindwa kufurukuta mbele ya ukuta wa Lipuli ulioongozwa na Mganda, Joseph Owino.
  Sare ya leo ya tatu na ya kwanza nyumbani – inaashiria benchi la Ufundi la Azam FC lina kazi ya kufanya kama lengo ni ubingwa wa Ligi Kuu ili kuweza kushindana na vigogo, Simba na Yanga.
  Mshambuliaji Donald Ngoma akimiliki mpira mbele ya beki Mganda wa Lipuli, Joseph Owino 

  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mbao FC ilierejea kileleni baada ya sare ya ugenini ya 1-1 na wenyei, Coastal Union Uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga. 
  Coastal Union ambayo imeendelea kukosa huduma ya mchezaji wake mpya, Ally Kiba ilitangulia kwa bao la Ayoub Lyanga dakika ya 31 kabla ya Said Khamis kuisawazishia Mbao FC dakika ya 50.  
  Na kwa sare hiyo, Mbao FC inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi saba, ikiishushia nafasi ya pili Mtibwa Sugar yenye poinyi 13 za mechi saba pia. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Kagera Sugar imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Mabao ya Kagera Sugar ya kocha Mecky Mexime leo yamefungwa na Ramadhani Kapera mawili, dakika za 47 na 86 na lingine Japhet Makalai dakika ya 52, wakati la Ndanda FC limefungwa na Mohamed Manzi dakika ya 59.
  Kwa ushindi huo, Kagera Sugar inafikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi sita, ikishinda mbili na kutoa sare nne, wakati Ndanda FC inabaki na pointi zake saba baada ya kucheza mechi saba.
  Nayo Stand United imelazimishwa sare ya bila kufungana na Tanzania Prisons ya Mbeya Uwanja wa CCM kambarage mjin Shinyanga. Stand United inafikisha pointi 11 baada ya kucheza mechi nane na Prisons inafikisha pointi saba katika mechi ya nane.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA AANZA KAZI AZAM FC YALAZIMISHWA SARE 0-0 NA LIPULI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top