• HABARI MPYA

  Tuesday, September 25, 2018

  HOMA YA PAMBANO LA WATANI; YANGA WAHAMA MJI, SIMBA SC BADO WAPO DAR

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  HOMA ya pambano la kwanza la msimu la Ligi Kuu ya Tanzania Bara la watani wa jadi inazidi kupanda na jana Yanga wamehama mji kuelekea Morogoro kwa maandalizi zaidi, huku Simba SC wakiwa bado wametulia Dar es Salaam.
  Nyasi za Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam zitatimbika Jumapili kwa mchezo mkali wa watani wa jadi nchini ambao unakuja mapema tu katika msimu wa 2018-2019.
  Yanga SC wameondoka jana kwenda ‘Mji Kasoro Bahari’ Morogoro kuweka kambi kujiandaa na mchezo huo, ikiwa ni siku moja tu baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Singida United kwenye mchezo mwingine wa Ligi Kuu Uwanja wa Taifa.

  Emmanuel Okwi wa Simb SC (kulia) na Kelvin Yondan (kushoto) katika mchezo uliopita Aprili 29

  Huo ulikuwa ushindi wa nne mfululizo katika mechi zote nne za mwazo za Ligi Kuu, baada ya awali kushinda 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, 4-3 dhidi ya Stand United na 1-0 dhidi ya Coastal Union, zote Uwanja wa Taifa.  
  Mahasimu wao Simba SC wanaweza kuingia kambini Jumatano na inawezekana ikawa Zanzibar kama kawaida yao. 
  Simba wanaonekana hawana presha na hii mechi na wachezaji wake hadi jana walikuwa mitaani na wengine walikwenda kibinafsi Uwanja wa Uhuru kuangalia mechi ya African Lyon na Mtibwa Sugar. 
  Ikumbukwe Simba SC wataingia kwenye mchezo huo wakitoka kucheza mechi tano, wameshinda tatu 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, 2-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa na 3-1 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, sare moja 0-0 na Ndanda FC mjini Mtwara na kufungwa moja, 1-0 na Mbao FC huko Mwanza.
  Huo utakuwa mchezo wa pili kuzikutanisha timu hizo mwaka huu, baada ya Aprili 29 Simba SC kushinda 1-0, bao pekee la Erasto Edward Nyoni dakika ya 37, mechi ya marudiano ya msimu uliopita wa Ligi Kuu. 
  Mechi ya kwanza ya msimu huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Oktoba 28 Uwanja wa Taifa Simba wakitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HOMA YA PAMBANO LA WATANI; YANGA WAHAMA MJI, SIMBA SC BADO WAPO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top