• HABARI MPYA

    Wednesday, September 26, 2018

    HAJATOKEA KAMA ABDALLAH ‘KING’ KIBADENI MECHI ZA WATANI WA JADI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NYASI za Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam zinatarajiwa kutimbika vya kutosha kwa mtanange wa watani wa jadi, Simba na Yanga kuanzia Saa 11:00 jioni.
    Kucheza Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki mechi baina ya timu hizo.
    Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine, hupewa zawadi kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
    Wapo waliolewa sifa au kujisahau na kupotea kwenye ramani ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao mfululizo kwenye mechi za watani.
    Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere (sasa marehemu, wa pili kulia) akimsabahi Abdallah Kibadeni (wa pili kushoto) enzi zake

    Said Sued 'Scud' alifunga bao pekee la ushindi kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi Kuu Mei 18, mwaka 1991.
    Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
    Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991, jambo ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.
    Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 1992 na huo ukawa mwisho wa umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.
    Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kazi kubwa sana katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani Abdallah Athumani Seif, maarufu kama King Kibadeni, au Ndululu kama walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la kujivunia katika historia ya mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi sasa halijavunjwa.
    Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi sasa aliyeweza kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi za watani wa jadi katika Ligi.
    Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga ilipotandikwa mabao 6-0 na Simba.
    Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi, yakitiwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine Selemani Sanga wa Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
    Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa ana sherehe binafsi za kutumbukiza mabao matatu peke yake kwenye mechi baina ya watani hao, jambo ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za Simba au Yanga.
    Tangu hapo zimefuatia mechi nyingi za Simba na Yanga, vizazi tofauti lakini hakuna mchezaji aliyethubutu kufikia rekodi ya Mzee Kibadeni. 
    Wapo waliokaribia, kwa kuishia kwenye mabao mawili, hao ni pamoja na James Tungaraza, Iddi Moshi wa Yanga, Mark Sirengo na Emmanuel Okwi wa Simba, lakini si kufikisha mabao matatu.
    Okwi alipata nafasi nzuri ya kuvunja rekodi ya King Kibadeni Mei 6, mwaka 2012 Simba SC ikiichapa Yanga mabao 5-0, lakini baada ya kufunga mabao mawili dakika ya pili na 62, hakulazimisha kupiga penalti tatu alizozisababisha mwenyewe akawaachia Mzambia Felix Sunzu kufunga dakika ya 56, kipa Juma Kaseja dakika ya 67 na kiungo Patrick Mafisango (sasa marehemu) dakika ya 72.
    Okwi ambaye aliwahi kucheza Yanga pia na akawafunga Simba, Jumapili anatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Wekundu wa Msimbazi akiwa na Mnyarwanda, Meddie Kagere, ambaye kiasili anatokea Uganda pia.
    Upande wa Yanga, kurejea kwa Mrundi Amissi Tambwe kunamaanisha anaweza akacheza pamoja na Mkongo, Heritier Makambo, safu za ushambuliaji za timu zote zikiongozwa na wachezaji wa kigeni. Tutarajie rekodi ya Kibadeni kuvunjwa, au bado mlima mrefu?
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJATOKEA KAMA ABDALLAH ‘KING’ KIBADENI MECHI ZA WATANI WA JADI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top