• HABARI MPYA

  Friday, September 28, 2018

  MASHABIKI WATAKAOHUDHURIA PAMBANO LA SIMBA NA YANGA JUMAPILI KUPIMWA AFYA

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  MASHABIKI watakaojitokeza kushuhudia mchezo wa watani wa jadi, Simba na Yanga watapata huduma ya kupimwa magonjwa mbalimbali ili kutambua afya zao. 
  Wizara ya Afya imeamua kusogeza huduma zake katika mchezo huo kwa sababu unavutia watu mashabiki wengi, hivyo inaamini watawafikia Watanzania wengi kwa urahisi zaidi.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Afya kwa Umma, Ama Kasangala amesema kwamba kupitia kampeni yao ya Furahia Kandanda, Lakini Je Unajua Afya Yako? Pima Jitambue Ishi watakuwepo katika maeneo maalum waliyotenga kwa ajili ya watu kwenda kujua afya zao.

  “Simba na Yanga zina mashabiki wengi, hivyo tumeamua kusogeza huduma zetu jirani, huduma yetu ya kwanza itakua kuchangia damu, kupima kuhusu magonjwa mbalimbali na kutoa elimu ya afya, tutakuwa na sehemu tatu za kutoa huduma hizi ya kwanza itakua upande wa Simba ya pili Yanga na tatu  itakaa katikati,” amesema Naibu huyo.
  Katika mchezo huo Waziri wa Afya,  Ummy Mwalimu anatarajiwa kumkabidhi kampeni hiyo Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe kampeni hiyo iliyozinduliwa mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
  Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendelea ya Michezo, Dk. Yussuph Singo amesema kwamba ulinzi umeimarishwa zaidi katika mchezo huo, hivyo mashabiki watakaokwenda uwanjani kwa ajili ya kufanya vurugu watadhibitiwa.
  “Tumekuwa na vikao zaidi ya vinne vya maandalizi ya mechi ya Jumapili, tunajua ni Derby lakini pia ni mchezo mkubwa kwa vilabu hivi viwili vyenye mashabiki wengi, tumejipanga vizuri na watu wa usalama,".
  "Nitoe rai kwa wale wenzetu wanaokuja uwanjani kwa ajili ya kufanya fujo, kamera zetu hapa uwanjani (CCTV) zinafanya kazi vizuri sana yoyote atakayefanya vitu viovu tutambaini, hatutarajii tena mambo ya uvunjaji viti na wizi wa koki kutokea,”amesema Mkurugenzi huyo.
  Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema kwamba tiketi za kushuhududia mtanange huo zitakuwa zinauzwa maeneo ya jirani na uwanja huo.
  “Naomba niseme kuelekea mchezo huu hakuna tiketi itakayouzwa uwanja wa Taifa, tumetenga maeneo jirani na Uwanja huu yatakayotumika kuuzia tiketi hizo, maeneo hayo ni, DUCE, Uhasibu (TIA) na wale wanaotokea maeneo ya Temeke na Chang’ombe tiketi zitapatikana Hotel ya PR, niweke wazi kuwa hakuna mtu yeyote atakayekatiza eneo la Uwanja wa taifa bila tiketi,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MASHABIKI WATAKAOHUDHURIA PAMBANO LA SIMBA NA YANGA JUMAPILI KUPIMWA AFYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top