• HABARI MPYA

  Sunday, September 23, 2018

  TAMBWE AFUFUA MAKALI, AFUNGA MABAO YOTE YANGA SC YAICHAPA SINGIDA UNITED 2-0 TAIFA

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Yanga SC imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida United usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Shujaa wa Yanga leo ni mshambuliaji wake mkongwe, Mrundi Amissi Joselyn Tambwe aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha kwanza na sasa wana Jangwani hao wanafikisha pointi 12 baada ya kushinda mechi zao zote nne za mwanzo.
  Tambwe ambaye karibu msimu wote uliopita hakucheza kwa sababu alikuwa anasumbuliwa na maumivu, alifunga bao la kwanza dakika ya 29 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Ibrahim Ajib Migomba waliyekuwa naye Simba SC kabla ya kuhamia Yanga kwa wakati tofauti.
  Tambwe tena akaifungia Yanga SC bao la pili dakika ya 45 kwa shuti kali kutoka umbali wa mita 12 baada ya pasi nzuri ya beki wa kushoto, Gardiel Michael Mbaga.

  Amissi Tambwe (kushoto) akiwa na Matheo Anthony baada ya kufunga leo

  Kipindi cha pili Singida United walibadilika na kuanza kuwashambuliaji Yanga SC hususan baada ya kumuingiza mshambuliaji wake hatari, Habib Hajji Kiyombo, lakini sifa zimuendee kipa Beno Kakolanya aliyeokoa vizuri michomo miwili ya hatari ya mchezaji huyo.
  Baada ya mchezo huo, Yanga SC wanakwenda kambini kujiandaa na mchezo dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Jumapili.
  Simba SC nayo leo imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, kuashiria kwamba kuelekea pambano la watani mambo ni moto. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Beno Kakolanya, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Andrew Vincent ‘Dante’, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Deus Kaseke/Said Makapu dk76, Papy Kabamba Tshishimbi, Amissi Tambwe/Yussuph Mhilu dk83, Ibrahim Ajib na Matheo Antony. 
  Singida: David Kisu, Kennedy Juma, Mohammed Tello, Elisha Muroiwa, Rajab Zahir, Yussuph Ngoma, Athanas Mdam/ Habibu Kiyombo dk53, Amara Diaby, Hans Kwofie, Kenny Ally/Tiber John dk71 na Geoffrey Mwashiuya Awesu Awesu dk53.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAMBWE AFUFUA MAKALI, AFUNGA MABAO YOTE YANGA SC YAICHAPA SINGIDA UNITED 2-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top