• HABARI MPYA

  Thursday, September 27, 2018

  SAMATTA AIZUNGUMZIA MECHI YA SIMBA NA YANGA MOJA TU ALIYOCHEZA, ASEMA NJE NA NDANI…

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba anajivunia kuwa mmoja wa wachezaji waliowahi kucheza mechi ya Simba na Yanga, kwani huo ni mchezo wa aina yake na wa heshima kwa mchezaji anapofanya vizuri.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online katika mahojiano maalum yaliyofanyika kwa simu, Samatta amesema kwamba alicheza mechi ya watani akiwa mchezaji wa Simba SC Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Samatta alianza na mechi hiyo ikaisha kwa sare ya 1-1, Yanga SC wakitangulia kwa bao la penalti la beki wa kushoto, Stefano Mwasyika dakika ya 59, kabla ya Mussa Hassan Mgosi kuisawazishia Simba SC kwa bao la utata dakika ya 73.

  Mbwana Samatta (kushoto) akiwa na mchezaji mwenzake wa timu ya taifa, Simon Msuva 

  Utata ulitokana na refa Orden Mbaga kwanza kulikataa bao hilo kabla ya kulikubali baada ya Mgosi kumuambia aangalie marudio ya picha za kamera kubwa uwanjani iliyokuwa inaonyesha mechi hiyo na baada ya hapo akaenda ya kujadiliana na msaidia wake namba moja ndipo akaweka mpira kati.
  “Kama wachezaji wengine, nilipenda kuwa kwenye vichwa vya habari baada ya mchezo, nilipenda kucheza kwa kiwango kikubwa, kuisaidia timu kupata ushindi, uweze kuwapa furaha mashabiki wa timu yangu, kwan fikira zangu ziliniambia hakuna furaha kubwa watakayopata kama kuwafunga watani wa jadi,”alisema Samatta akizungumzia ushiriki wake mechi ya Machi 5, mwaka 2011.
  Hata hivyo, Samatta ambaye kwa sasa anachezea KRC Genk ya Ubelgiji aliyojiuga nayo Januari mwka 2016 akitokea TP Mazembe ya DRC iliyomtoa Simba SC mwaka 2011, amesema kwamba alichojifunza ni kwamba mechi ya watani ndani uwanja inakuwa tofauti kabisa na nje.
  “Ni kwamba nje ya Uwanja presha huwa ni kubwa, kutoka kwa viongozi pamoja na mashabiki, lakini ndani ya Uwanja kunakuwa hakuna presha kubwa na kunakuwa na maongezi mengi ya kirafiki ndani ya Uwanja baina ya wachezaji wa timu zote,”amesema. 

  Mbwana Samatta alipokuwa Simba SC mwaka 2011 hapa anashangilia bao alilofunga na mchezaji mwenzake, Juma Jabu (kulia) 

  Mbwana Samatta (kushoto) akiichezea TP Mazembe katika klabu Bingwa ya Dunia Japan mwaka 2015

  Mbwana Samatta kwa sasa anatamba KRC Genk ya Ubelgiji baada ya kufikia kilele cha mafanikio Afrika 

  Samatta alidumu kwa msimu mmoja tu Simba SC baada ya kusajiliwa kutoka African Lyon, kabla ya kuchukuliwa na TP Mazembe ambako alipata mafanikio makubwa hadi kununuliwa Ulaya.
  Akiwa Mazembe aliisaidia timu hiyo kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Afrika naye akawa mfungaji Bora, hivyo kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika. 
  Na tangu ametua Genk, Samatta amekwishacheza jumla ya mechi 119 za mashindano yote na kufunga mabao 43.
  Katika Ligi ya Ubelgiji amecheza mechi 93 na kufunga mabao 29, Kombe la Ubelgiji mechi nane mabao mawili na Europa League mechi 18 mabao 12.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AIZUNGUMZIA MECHI YA SIMBA NA YANGA MOJA TU ALIYOCHEZA, ASEMA NJE NA NDANI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top