• HABARI MPYA

  Friday, September 28, 2018

  HAIJAWAHI KUTOKEA SIMBA NA YANGA TAMU KULIKO HIII LIPIGWA NYAMAGANA 1974 ENZI NA AKINA MANARA NA MAMBOSASA

  Na mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  NYASI za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zinatarajiwa kuwaka moto Jumapili kwa mpambano wa Ligi Kuu Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Katika mfululizo wa makala za kuelekea pambano la watani wa jadi Jumapili, leo tunahamia kwenye mchezo mzuri zaidi kuwahi kutokea kihistoria baina ya michezo iliyowahi kuwakutanisha wapinzani hao wa jadi. 
  Kuna mechi Simba iliifunga Yanga 6-0 na kila timu imewahi kushinda 5-0. Lakini kwa mujibu wa wazoefu wa kushuhudia mechi baina ya miamba hiyo, haujawahi kutokea mchezo mkali wa Simba na Yanga kama ule wa Agosti 10, mwaka 1974.
  Huo ulifanyika katika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza ukiwa ni mchezo wa Fainali ya Klabu Bingwa ya Taifa na Yanga wakatoka nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 2-1 baada ya dakika 120.
  Mapema dakika ya 16, Adam Sabu (sasa marehemu) aliyekuwa akiitwa Gerd Muller akifananishwa na mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Ujerumani, aliifungia Simba bao la kuongoza ambalo lilidumu hadi kipindi cha pili.
  Wakati baadhi ya watu wanaanza kuinuka kwenye Uwanja wa Nyamagana, wakiamini Simba SC imetetea ubingwa wake kwa bao pekee la Sabu, mshambuliaji aliyekuwa ana misuli ya nguvu ya kufumua mashuti makali, Gibson Sembuli (sasa marehemu pia) akaisawazishia Yanga, zikiwa zimebaki dakika tatu mchezo kumalizika, yaani dakika ya 87.
  Kwa sababu huyo, mchezo ukahamia kwenye dakika 30 za nyongeza na katika dakika ya saba ya muda huo, mchezaji bora kabisa kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania daima, Sunday Manara ‘Computer’ akaifungia Yanga bao la pili na la ushindi dakika ya 97.
  Yanga ikarejesha ubingwa wake, kwa ushindi wa 2-1 katika pambano la kwanza kabisa baina ya watani wa jadi kufanyika nje ya ardhi ya Dar es Salaam.

  Kipa wa Simba SC, Athumani Mambosasa (sasa marehemu, juu kulia) akiwa amedaka mpira mbele ya mshambuliaji wa Yanga SC, Kitwana Manara 'Popat', huku akilindwa na beki wake, Jumanne Hassan 'Masimenti' kulia Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza, Agosti 10, mwaka 1974 

  KWA NINI PAMBANO BORA ZAIDI LA WATANI?
  KATIKA kujiandaa na msimu wa 1974, Simba SC walifanya ziara ya mafunzo nchini Poland, wakati Yanga SC nao walikwenda Romania.
  Lakini pia, kikosi cha Simba SC ni ambacho kilitwaa ubingwa msimu uliotangulia mwaka 1973 na pia ndicho kilitwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati mwaka 1974 pamoja na kufika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka huo, wakatolewa na Mehallal El Kubra ya Misri, wakitoka kuwatoa Hearts Of Oak ya Ghana.
  Kwa Yanga, kikosi chao kilikuwa kinaundwa na nyota wengi walioifikisha timu hiyo Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo, 1969 na 1970 mara zote ikitolewa na Asante Kotoko ya Ghana kwa mbinde- hivyo ukichanganya na mazoezi ya Poland na Romania, timu hizo zilikuwa moto.  
  Timu hizo ziliporejea nchini, zikakutana katika kituo cha mwaka huo cha Klabu Bingwa ya Taifa, mjini Mwanza enzi hizo ligi ikichezwa katika mtindo kama wa Kombe la Taifa, kunakuwa na kituo na makundi mawili na baadaye washindi wa makundi wanakutana katika fainali.
  Simba na Yanga ziliongoza makundi yao na zikakutana katika fainali mjini Mwanza, mchezo ambao ulikuwa gumzo mno- mamia walisafiri kutoka mikoa mbalimbali kuelekea mjini Mwanza, wakiwemo wakazi wa Dar es Salaam. Mwanza ilifurika na Nyamagana hapakutosha.
  Wakati huo, Simba SC kambi yao ilikuwa katikati ya Jiji la Mwanza tu, hoteli moja maarufu enzi hizo, Sukumaland wakati Yanga walikuwa wanaweka kambi yao Butimba.
  Ikumbukwe katika mashindano ya mwaka huo, Simba SC ilimkosa kiungo wake mahiri, Khalid Abeid ambaye alikuwa majeruhi, lakini kwa mchecheto wa mechi hiyo, walitaka kumlazimisha kucheza, ila ikashindikana kwa sababu hakuwa fiti.
  Ilikuwa mechi kali na ya ushindani na siku hiyo, mshambuliaji wa Simba SC, Saad Ali alizirai uwanjani baada ya kupigwa na mpira uliopigwa na Sembuli, akakimbizwa hospitali, ambako ilielezwa hakupata fahamu hadi siku ya pili. Mbaya zaidi, usiku ilivumishwa Saad amefariki dunia, lakini alipona.
  Kuna uvumi fulani, eti sehemu ambayo aliangukia Saad paliota kichuguu ambacho miaka nenda, rudi hakipotei Nyamagana. 
  Aidha, mshambuliaji mwingine wa Simba SC, Willy Mwaijibe naye aligongana na kipa wa Yanga SC, Elias Michael ‘Nyoka Mweusi’ na wakaumia wote na kutoka nje. Nafasi ya Mwaijibe aliingia Adam Sekulu na nafasi ya Michael aliingia Muhiddin Fadhil.
  Walioshuhudia wanasema soka ilichezwa Nyamagana Agosti 10 ya mwaka 1974, enzi hizo Simba na Yanga, Simba na Yanga kweli kuanzia wachezaji, viongozi hadi wapenzi. Hadi tunaingia katika milenia mpya, bado haijatokea mechi nyingine ya kufananishwa na hiyo.
  Katika mchezo huo, vikosi vilikuwa; Yanga SC; Elias Michael/Muhiddin Fadhil, Suleiman Sanga, Boy Wickens, Hassan Gobbos, Omar Kapera, Abdulrahman Juma, Leonard Chitete, Sunday Manara, Gibson Sembuli, Kitwana Manara na Maulid Dilunga.  
  Simba SC; Athumani Mambosasa, Shaaban Baraza, Mohamed Kajole, Jumanne Masimenti, Omar Chogo, Omar Gumbo, Wily Mwaijibe/Adam Sekulu, Haidari Abeid ‘Muchacho’, Adam Sabu, Abdallah Kibadeni na Saad Ally/Abbas Dilunga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAIJAWAHI KUTOKEA SIMBA NA YANGA TAMU KULIKO HIII LIPIGWA NYAMAGANA 1974 ENZI NA AKINA MANARA NA MAMBOSASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top