• HABARI MPYA

  Wednesday, September 26, 2018

  KOCHA MBELGIJI WA SIMBA SC ASEMA KWA NINI AMEKATAA KUPELEKA TIMU ZANZIBAR

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mbelgiji Patrick Aussems amesema anauchukulia kawaida mchezo dhidi ya Yanga SC na anauona ni sawa na michezo mingine ya Ligi Kuu Tanzania Bara waliocheza awali.
  Kuelekea mchezo huo utakayochezwa tarehe 30 siku ya Jumapili, Simba Sc wameendelea na mazoezi yao katika Uwanja wa Boko Veterani, ambao imekuwa sehemu yao mahsusi ya kujifua siku za karibuni.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya mazoezi ya leo, Mbelgiji huyo amesema kwamba haoni tofauti ya kufanya mazoezi Dar es Salaam ama nje ya mkoa au nchi, kwa sababu mtanange huo anauchukulia sawa na mingine.
  "Nini tofauti ya kuweka kambi hapa na nje ya hapa, kwangu mimi sioni utofauti wowote, mchezo huu ni wakaida kama michezo mingine,"alisema Kocha Aussems ambaye ana matarajio makubwa ya ushindi.

  Kocha Patrick J. Aussems (kushoto) na Wasaidizi wake, Mrundi Masoud Juma (katikati) na Mtunisia Adel Zrane (kulia) wote walikuwepo mazoezini leo Uwanja wa Boko PICHA YA MAKTABA 

  "Najua mchezo huu ni maalum kwa mashabiki wa Yanga na Simba, lakini tumejipanga kushinda, hakuna timu inayoingia uwanjani kwa mategemeo ya kushindwa hata tungekua tunacheza Lipuli au Liverpool, Real Madrid mategemeo yetu ni kushinda,".
  Kwa kawaida kumekuwa na maandalizi maalumu kwa timu hizi mbili zinapokaribia kukutana katika michezo ya mashindano mbalimbali na mara nyingi kambi huwa nje Dar es Salaam na hata nje ya nchi. 
  Wakati mahasimu wao Yanga wamekwenda Morogoro, Simba SC ambayo imewahi hadi kwenda Afrika Kusini kwa maandalizi ya mechi hizi safari hii imebaki tu Dar es Salaam.
  Na inaelezwa utashi wa uongozi ulikuwa ni kuipeleka timu Zanzibar kama ilivyo kawaida yao, lakini Mwalimu Aussems amekataa akisema anahofia kuwachosha wachezaji.
  Wachezaji wote waliosajiliwa na Simba SC msimu huu wamefanya mazoezi leo chini ya Kocha Aussems na Wasaidizi wake, Mrundi Masoud Juma, Mtunisia Adel Zrane kocha wa mazoezi ya nguvu na mzalendo, Muharami Mohammed 'Shilton', kocha wa makipa  isipokuwa viungo wa zamani wa Mtibwa Sugar, Hassan Dilunga na Muzamil Yassin ambao ni majeruhi.
  Ikumbukwe katika mchezo huyo Simba itamkosa Nahodha wake, mshambuliaji John Bocco ambaye atakuwa anatumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mechi dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga siku ambayo alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-1.
  Yanga inashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu, ikiwana pointi 12 baada ya kushinda mechi zake zote za mwanzo, nyuma ya Mbao FC yenye pointi 13 za mechi sita, wakati Simba SC yenye pointi 10 za mechi tano ni ya nne, nyuma ya Azam FC yenye pointi 12  za mechi tano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA MBELGIJI WA SIMBA SC ASEMA KWA NINI AMEKATAA KUPELEKA TIMU ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top