• HABARI MPYA

  Sunday, September 23, 2018

  AZAM FC YAPATA USHINDI WA KWANZA UGENINI, YAICHAPA ALLIANCE FC 1-0 MWANZA

  Na Michael Mayalla, MWANZA
  AZAM FC imepata ushindi wa kwanza katika mechi zake za ugenini baada ya kuichapa 1-0 Alliance FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Shukrani kwake mfungaji wa bao hilo pekee, kiungo Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu dakika ya 59 na sasa timu hiyo ya Aljah Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inafikisha pointi 11 baada ya mechi tano.
  Azam FC imeshinda mchezo wa leo ikitoka kutoa sare mbili mfululizo, 1-1 na Mwadui huko Kishapu mkoani Shinyanga na 0-0 na Biashara United huko Musoma mkoani Mara.
  Na hiyo ni baada ya mwanzo mzuri wakishinda mechi zao mbili za kwanza nyumbani, 2-0 na Mbeya City na 3-0 na Ndanda FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo, Mbeya City imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Kiungo Mzimbabwe Tafadzwa Kutinyu ameifungia bao pekee Azam FC leo dakika ya 59

  Mbeya City ilitangulia kwa bao la Eliud Ambokile dakika ya 34 kabla ya Suleiman Mangoma kuwasawazishia Kagera Sugar dakika ya 52. 
  Mabingwa watetezi, Simba SC wakaibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya wenyeji, Mwadui FC Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Nahodha wake John Bocco akifunga mabao mawili kipindi cha kwanza kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili.
  Ushindi huo unarejesha amani Simba SC baada ya timu kucheza mechi mbili zilizopita bila kushinda, ikitoa sare ya 0-0 na Ndanda FC mjini Mtwara na kufungwa 1-0 na Mbao FC mjini Mwanza.
  Simba SC sasa inafikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi tano kuelekea pambano dhidi ya watani wa jadi, Yanga Jumapili Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Bocco ambaye atakosa mechi dhidi ya Yanga Septemba 30, alifunga bao la kwanza kwa penalti dakika ya 41 baada ya kiungo Shiza Kichuya kuangushwa na Miraj Maka kwenye boksi dakika ya 40.
  Bocco akaweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufikisha mabao 100 kwenye Ligi Kuu tangu imeanzishwa mwaka 1996, baada ya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 45, akimalizia pasi ya beki wa kulia, Shomari Kapombe kufuatia krosi ya mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.
  Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tangu amewasili kutoka Gor Mahia ya Kenya akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 50 kwa shuti kali kutoka umbali wa mita 16 baada ya kuwazidi mabeki wa Mwadui FC.
  Nahodha Bocco akatolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja dakika ya 80 baada ya kumpiga ngumi beki wa Mwadui FC, Revocatus Richard wakati wawili hao wakigombea mpira.
  Na Mwadui FC wakatumia fursa hiyo kujipatia bao la kufutia machozi kwa shambulizi la kushitukiza, mfungaji Charles Ilamfya dakika ya 81 baada ya kumzidi mbio na ujanja, beki wa Simba SC, Serge Wawa Pascal.
  Mechi ya mwisho ya Ligi Kuu leo inaendelea hivi sasa Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kati ya wenyeji, Yanga SC dhidi ya Singida United. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAPATA USHINDI WA KWANZA UGENINI, YAICHAPA ALLIANCE FC 1-0 MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top