• HABARI MPYA

  Sunday, September 30, 2018

  MECHI YA MAHASIMU WA JADI, SIMBA NA YANGA YAMALIZIKA KWA SARE 0-0 UWANJA WA TAIFA

  Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baina ya watani wa jadi, Simba na Yanga SC umemalizika kwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jioni ya leo.
  Kwa sare hiyo, Yanga SC inajisogeza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kutokana na kujiongezea pointi moja na kufikisha 13 baada ya kucheza mechi tano, nne nyingine zote wakishinda.
  Kwa upande wao, mabingwa watetezi, Simba SC wanafikisha pointi 11 baada ya kucheza mechi sita, wakitoa sare ya pili leo na kufungwa moja, nyingine tatu wakishinda.
  Lakini Simba SC watajilaumu wenyewe kwa kushindwa kuondoka na pointi zote kwenye mchezo wa leo, kwani walifanikiwa kuwazidi wapinzani wao muda wote. 
  Emmanuel Okwi (kushoto) akizungumza na Beno Kakolanya wakati mchezo ukiendelea leo Uwanja wa Taifa

  Simba SC walikuwa wana safu nzuri ya ulinzi iliyozuia mashambulizi machache ya kubahatisha ya Yanga – na safu yao ya kiungo ikafanya kazi nzuri ya kutengeneza nafasi, lakini washambuliaji wakashindwa kutimiza wajibu wao.
  Washambuliaji wa Simba SC, Mganda Emmanuel Okwi na Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere walikosa utulivu na ubunifu katika mchezo wa leo, zaidi wakilazimisha mambo.
  Nahodha wa Yanga SC, Kelvin Patrick Yondan pamoja na kuonyeshwa kadi ya njano mapema kipindi cha kwanza, lakini alitulia na kumalizia mchezo vizuri.
  Viungo wa Yanga SC, Deus Kaseke, Feisal Salum, Ibrahim Hajib na Papy Kabamba Tshishimbi walizidiwa kabisa na viungo wa Simba SC, Mzambia Cletus Chama, Mghana James Kotei na wazalendo Jonas Mkude na Shiza Kichuya.
  Sifa zaidi kwa upande wa Yanga zimuendee kipa Benno Kakolanya aliyedaka kwa ustadi wa hali ya juu na kuokoa hatari nyingi.
  Kakolanya alitokea vizuri na kuokoa kwa mguu akiutoa mpira nje dakika ya 11 wakati Okwi akijiandaa kufunga kufuatia pasi nzuri ya Shiza Kichuya baada ya Simba SC kugongeana vziuri.
  Dakika ya 21 Kichuya naye akapiga juu ya lango akiwa kwenye nafasi nzuri baada ya krosi nzuri ya Shomari Kapombe kumpita Okwi.
  Dakika ya 28 Okwi alikutana na mpira uliorudi kufuatia kuokolewa na Kakolanya baada ya shuti la Kagere aliyekuwa tayari ameotea, lakini refa Deonisya Rukyaa akawa makini na kutowapa Simba bao haramu.
  Dakika ya 56 kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi akapiga juu ya lango akiwa kwenye nafasi nzuri kufuatia pasi nzuri ya kiungo Deus Kaseke, hiyo ilikuwa nafasi nzuri kwa Yanga kwenye mchezo wa leo.
  Mshambuliaji Mkongo, Heritier Makambo aliyekuwa peke yake mbele ya lango la Simba SC leo hakupata huduma nzuri kutoka kwa viungo wake na kujikuta akiwa mtalii uwanjani.
  Kwa ujumla, Simba SC walitawala mchezo wa leo na hata baada ya kuingia kwa Said Ndemla, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na Adam Salamba bado mambo hayakugeuka.
  Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, James Kotei, Jonas Mkude, Cletus Chama/Said Ndemla dk81, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/Adam Salamba dk88 na Shiza Kichuya/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk62.
  Yanga SC; Beno Kakolanya, Paulo Godfrey, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Abdallah Shaibu 'Ninja', Dues Kaseke/Mrisho Ngassa dk78, Papy Kabamba Tshishimbi, Haritier Makambo, Feisal Salum na Ibrahim Ajib/Matheo Anthony dk55.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI YA MAHASIMU WA JADI, SIMBA NA YANGA YAMALIZIKA KWA SARE 0-0 UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top