• HABARI MPYA

    Sunday, September 30, 2018

    KUELEKEA PAMBANO LA WATANI SAA 11:00 JIONI TAIFA; SIMBA SC WANATOKEA MBEZI BEACH, YANGA WANATOKEA MANZESE

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    WATANI wa jadi wanaingia kwenye mchezo wa leo wakitoka kwenye mazingira tofauti, Yanga SC wakitokea Manzese na Simba SC wakitokea Kunduchi.  
    Kwa wiki yote, Yanga SC walikuwa kambini mjini Morogoro kabla ya jana kufikia katika hoteli ya Nefaland, eneo la Argentina kitongoji cha Manzese kwa maandalizi ya mwisho mwisho.
    Simba SC wao wiki yote hii wamekuwa katika hoteli ya Sea Scape eneo la Kunduchi, au Mbezi Beach wakifanya mazoezi yao Uwanja wa Boko Veterani. 
    Watani wa jadi, Simba na Yanga watamenyana Uwanja wa Taifa kuanzia Saa 11:00 jioni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambao utahudhuriwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai.
    Juu ni hoteli ya Sea Scape wanayotokea Simba na chini ni hoteli ya Nefaland wanayotokea Yanga

    Mechi hiyo itachezeshwa na refa Jeonisya Rukyaa kutoka Kagera akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono wa Dar es Salaam pembezoni mwa Uwanja na Mezani atakuwepo Elly Sasii.
    Jeonesia Rukyaa, refa wa Kagera tayari ana uzoefu wa kupuliza kipyenga katika michezo ya watani wa jadi, baada ya awali kuchezesha mechi mbili.
    Kwanza ilikuwa Desemba 13, mwaka 2014 mechi ya Mtani Jembe, Simba SC wakishinda 2-0, mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri na ya pili Februari 20, mwaka 2016 Yanga SC wakishinda 2-0, mabao ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe. 
    Mchezo wa kesho utakuwa wa pili kuzikutanisha timu hizo mwaka huu, baada ya Aprili 29 Simba SC kushinda 1-0, bao pekee la Erasto Edward Nyoni dakika ya 37, mechi ya marudiano ya msimu uliopita wa Ligi Kuu. 
    Mechi ya kwanza ya msimu huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1 Oktoba 28 Uwanja wa Taifa Simba wakitangulia kwa bao la Shiza Kichuya dakika ya 57, kabla ya Obrey Chirwa kuisawazishia Yanga dakika ya 60.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUELEKEA PAMBANO LA WATANI SAA 11:00 JIONI TAIFA; SIMBA SC WANATOKEA MBEZI BEACH, YANGA WANATOKEA MANZESE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top