• HABARI MPYA

  Saturday, September 22, 2018

  KIDAU AMPA SIKU TATU WAKILI KUULI KUJIELEZA KWA NINI AMESIMAMISHA UCHAGUZI WA SIMBA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limempa siku tatu kuanzia Septemba 19, Mwenyekiti wa Kamati yake ya Uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli kujieleza juu ya kuusimamisha Uchaguzi wa klabu ya Simba SC uliopangwa kufanyika Novemba 3, mwaka huu.
  Katika barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau Kuuli ametakiwa kujieleza kama uamuzi wake wa kuusimamisha uchaguzi wa Simba SC umetokana na kikao cha Kamati yake cha Dodoma.
  Kidau amesema katika barua kwamba walifanya kikao mjini Dodoma kupitia kalenda ya uchaguzi ya Bodi ya Ligi na marekebisho ya kufanya katika uchaguzi wa Simba, lakini haikuelekezwa mchakato huo usimamishwe.

  Wilfred Kidau (kushoto) amemempa siku tatu Wakili Revocatus Kuuli kujieleza juu ya kuusimamisha Uchaguzi wa Simba SC 

  “Shirikisho la Mpira wa Miguu limesikia ukiongea na vyombo vya Habari kuhusiana na kusimamishwa kwa uchaguzi wa Simba unaotarajiwa kufanyika, Shirikisho la Mpira wa Miguu linataka kujua umetoa wapi mamlaka ya kuongea na vyombo vya Habari bila kuwasiliana na Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu,”amesema Kidau.
  Aidha, kiungo huyo wa zamani wa Simba SC amesema kwamba akiwa msimamizi wa Sekretarieti ambayo moja ya majukumu yake ni kuratibu mawasiliano yote ya Kamati na Wanachama wake, anataka kujua Kuuli ametoa wapi mamlaka ya kuwasiliana moja kwa moja na Sekretarieti ya Simba SC bila kupitia ofisi ya Katibu Mkuu wa TFF.  
  Ikumbukwe, Septemba 17, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Kuuli alisitisha uchaguzi wa Simba kutokana na kukiukwa kwa baadhi ya taratibu za msingi. Lakini siku mbili baadaye ikaripotiwa ameruhusu uchaguzi huo uendelee baada ya dosari zilizojitokeza kufanyiwa marekebisho.
  Na jana Simba ikatangaza majina ya wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, huku nafasi ya Mwenyekiti wakipitishwa wote walioomba, Swedy Nkwabi na Mtemi Ramadhani.
  Katika nafasi za Ujumbe wa Bodi waliopitishwa ni Hussein Kitta Mlinga, Iddy Noor Kajuna, Mohamed Wandi, Suleiman Haruob Said, Abdallah Rashid Mgomba, Christopher Kabalika Mwansasu na Alfred Martin Elia.
  Wengine ni Ally Suru, Mwina Mohamed Kaduguda, Said Tully, Juma Abbas Pinto, Hamisi Ramadhani Mkoma, Abubakari Zebo na Patrick Paul Rweyemamu, Zawadi Ally Kadunda wakati nafasi ya Wajumbe Wanawake wamepitishwa Asha Ramadhani Baraka na Jasmine Badar Soudy.
  Walioenguliwa ni wawili tu, Selemani Omari Selemani na Omar Juma Mazola na Kamati ya Uchaguzi imesema leo itaanza kupokea pingamizi juu ya wagombea wa nafasi mbalimbali waliopitishwa hadi Septemba 23 na kila pingamizi litalipiwa Sh 50,000 na zitalipwa kupitia akaunti ya klabu.
  Uchaguzi wa Simba SC unakuja baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wao.
  Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
  Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua Salum Abdallah ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi Mkuu ujao.
  Katiba mpya ya Simba SC inaelekea Rais wa klabu awe na elimu ya kiwango cha Shahada ambaye ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake.
  Na Mwenyekiti huyo atakuwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
  Hiyo ni baada ya mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
  Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
  Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KIDAU AMPA SIKU TATU WAKILI KUULI KUJIELEZA KWA NINI AMESIMAMISHA UCHAGUZI WA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top