• HABARI MPYA

  Sunday, September 30, 2018

  NGOMA: NIMEFURAHI SANA KURUDI UWANJANI SASA SUBIRINI NIKAE SAWA MUONE KAZI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BAADA ya jana kucheza mechi yake ya kwanza Azam FC akitokea kwenye majeruhi, mshambuliaji Donald Ngoma, ameonesha kufurahishwa sana huku akiwaahidi makubwa mashabiki wa timu hiyo.
  Azam FC iliyokuwa ikicheza na Lipuli jana usiku na kutoka suluhu, ilishuhudiwa Ngoma akiingia dakika ya 62 kuchukua nafasi ya kiungo mkabaji Mudathir Yahya, mchezo huo pia ukiwa ni wa kwanza kwake tokea asajiliwe na timu hiyo msimu huu akitokea Yanga.  
  Licha ya kutoka kwenye majeraha ya takribani mwaka mmoja, Ngoma alionekana kuanza vema jana mechi yake ya kwanza akicheza kwa kujituma na kupambana na mabeki wa Lipuli huku akipata nafasi muhimu mbili za kufunga moja ikiwa ni ile ya kuangushwa katika eneo la hatari na kipa.
  Akizungumza baada ya mchezo huo Ngoma alisema anasikia furaha sana kurudi uwanjani baada ya kutoka kwenye majeruhi licha ya timu yake kutopata ushindi dhidi ya Lipuli.
  “Azam imenifanyia vitu vikubwa sana na mimi nimefurahi sana kuwa hapa, kuvaa jezi ya Azam, ni kitu kizuri na nimefurahi sana kwa mechi yangu ya kwanza, nafikiri tunatakiwa kuchukua pointi zaidi.
  “Tunakiwa kushinda mechi zaidi hususani mechi za nyumbani, tunatakiwa kupata pointi zinazohitajika, nafikiri tunatakiwa kujiboresha tunatakiwa kufanya vizuri zaidi, tunatakiwa kushinda haswa mechi za nyumbani,” alisema.
  Ngoma anayevalia jezi namba 11, alizungumzia mchezo huo kiujumla akidai walitengeneza nafasi kadhaa za kufunga mabao lakini haikuwa siku yao kutokana na kukosa bahati ya kufunga.
  “Tulifanya kila jitihada kipindi cha pili na kupata nafasi mbili za wazi nilizopata mimi, nafasi nyingine huenda mwamuzi aliona sio penalti sikuona tukio vizuri kwa sababu ndio mimi niliyekua na mpira,” alisema.
  Mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe, aliwapa tano mashabiki wa timu hiyo akidai kuwa wamekuwa wakiwapa sapoti mwanzo mwisho licha ya kutowafurahisha katika mchezo huo.
  “Mashabiki wamekuwa wakifanya kazi nzuri unajua wamekuwa wakijaribu kutusukuma kila mara kwa bidii hata pale mambo yanapokuwa hayaendi vizuri hususani mechi ya leo tulitakiwa kuwapa furaha lakini kwa bahati mbaya hatukuweza kufanya hivyo lakini nawaahidi mambo mazuri yanakuja,” alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA: NIMEFURAHI SANA KURUDI UWANJANI SASA SUBIRINI NIKAE SAWA MUONE KAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top