• HABARI MPYA

  Saturday, September 22, 2018

  WYDAD CASABLANCA WAVULIWA UBINGWA WA AFRIKA NA ES SETIF

  TIMU ya Wydad Athletic Club imevuliwa ubingwa wa Afrika baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na ES Setif ya Algeria katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali usiku wa Ijumaa Uwanja wa Mohamed V mjini Casablanca nchini Morocco.
  Kwa matokeo hayo, Setif wanasonga mbele katika Nusu Fainali kwa ushindi wa 1-0 walioupata kwenye mchezo wa kwanza Ijumaa iliyopita Uwanja wa Mei 8, 1945 mjini Setif, siku hiyo, bao hilo pekee lilifungwa na beki Msenegal, Isla Daoudi Diomande.
  Mechi nyingine za marudiano za Robo Fainali leo, Esperance ya Tunisia imefanikiwa kwenda Nusu Fainali baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Etoile du Sahel, zote za Tunisia Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse.
  Bao pekee la Esperance katika mchezo wa leo limefungwa na kiungo Muivory Coast, Fousseny Coulibaly dakika ya 87 akimalizia pasi ya beki mkongwe wa umri wa miaka 31, Mtunisia, Sameh Derbali.

  Ushindi huo wa ugenini katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali unaifanya Esperance isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa 3-1 baada ya awali kushinda 2-1 Jumamosi kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Olimpiki wa Rade.
  Nayo C.D. Primeiro de Agosto ya Angola imeitoa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa mabao ya ugenini, baada ya Mazembe kulazimisha sare ya 1-1 Uwanja wa TP Mazembe mjini Lubumbashi.
  Mshambuliaji kinda wa miaka 20 wa DRC, Jackson Muleka aliifungia bao la kuongoza Mazembe mapema tu dakika ya 12, akimalizia pasi ya kiungo Muivory Coast, Christian Raoul Kouame Koffi.
  Lakini TP Mazembe ikashindwa kujilinda na kuwaruhusu wageni kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji Mkongo pia, Mongo Kipe Lumpala Bokamba dakika ya 34 akimalizia pasi ya mshambuliaji Muangola, Hermenegildo Costa Paulo Bartolomeu.
  Na kwa sababu mechi ya kwanza timu hizo zilitoka sare ya 0-0 Jumamosi Uwanja wa Estádio 11 de Novembro mjini Luanda, Primeiro de Agosto inakwenda Nusu Fainali kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya 1-1.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WYDAD CASABLANCA WAVULIWA UBINGWA WA AFRIKA NA ES SETIF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top