• HABARI MPYA

    Friday, September 28, 2018

    MSUVA: NILITAKA KUPIGWA NA MASHABIKI ETI NAIHUJUMU YANGA, LAKINI BAADAYE NIKAWAFURAHISHA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva amesema kwamba hawezi kusahau alitaka kupigwa na mashabiki wa Yanga wakimtuhumu anahujumu timu dhidi ya mahasimu wa jadi, Simba SC.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu jana usiku kutoka Morocco, Msuva alisema kwamba kuna siku mashabiki wa Yanga walimfanyia fujo yeye na kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima baada ya mechi dhidi ya Simba wakitaka kuwapiga kwa madai wanahujumu timu.  
    Msuva amesema kwamba mechi za mwanzo dhidi ya Simba SC zilikiwa zinampa tabu sana kwa sababu ukiachilia mbali alikuwa kijana mdogo sana na asiye na uzoefu, lakini pia kwa sababu ya presha ya mashabiki. 

    Simon Msuva hawezi kusahau alitaka kupigwa na mashabiki wa Yanga wakimtuhumu anaihujumu timu dhidi ya Simba SC

    “Ukiangalia Simba na Yanga ni timu kubwa Tanzania na zina mashabiki wengi, kwa hivyo zina presha na zina aina yake ya maandalizi yake, kwa maana hiyo mimi nilikuwa bado sijaanza kuzoea, lakini ilifika kipindi nikazoea, ukaona mwenyewe kuna mechi nyingine hata penalti nikawa napiga,” amesema.
    Lakini Msuva anasema kwamba mechi anayoikumbuka zaidi ni ya Aprili 19, mwaka 2014 ambayo aliinusuru Yanga kuchapwa baada ya kufunga bao la kusawazisha dakika ya 86 na kupata sare ya 1-1 kufuatia Haroun Chanongo kuanza kuifungia Simba SC dakika ya 76.
    “Kwanza unajua siku ya kuamkia mechi na Simba nilikuwa silali, yaani sipati usingizi nafikiria kesho nachezaje. Kwa hivyo mimi ile mechi kaka kwa upande wangu nilifurahi sana kufunga, tena katika mazingira ambayo muda tayari ulikuwa umeendea mwishoni na watu pia walikuwa hawaniamini kwamba ninaweza nikafanya, lakini nikaweza kufanya,”alisema. 

    Simon Msuva akimtoka Amri Kiemba katika mechi ya Simba na Yanga mwaka 2014 

    Msuva ambaye kwa sasa anachezea Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, amesema kwamba mechi hiyo ilimjengea hali ya kujiamini na akaanza kuona mashabiki wanamkubali kiasi kwamba baada ya hapo akawa amezizoea mechi za watani.
    “Kuna mechi tulipata penalti mapema tu dakika ya tano, wachezaji wote wakakataa kwenda kupiga, mimi nikachukua mpira nikapiga nikafunga goli. Kwa hiyo ni kitu ambacho kwa upande wangu kwanza nilikuwa nafurahi zaidi nikiifunga Simba kwa sababu ya kufuta dhana kwamba mimi napenda Simba. Hapana. Yaani nilikuwa ninataka niwadhihirishie siko hivyo wanavyofikiria wao,” alisema Msuva.
    Kwa ujumla katika kipindi chake cha miaka mitano ya kuwa Yanga SC, Msuva amecheza jumla ya mechi 12 za mahasimu wa jadi na kufunga mabao mawili kabla ya kuhamia Kaskazini mwa Afrika Juni mwaka jana kwenda kucheza soka rasmi ya kulipwa.
    Alifunga katika sare ya 1-1 Aprili 19, mwaka 2014, akafunga bao la kwanza kwanza kwa penalti dakika ya tano na Februari 26, mwaka 2017, Yanga SC wakifungwa 2-1 na Simba ambayo mabao yake yalifungwa na mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo dakika ya 66 na winga mzawa Shiza Kichuya dakika ya 81.

    Simon Msuva akimlamba chenga beki wa Mtibwa Sugar, Issa Rashid 'Baba Ubaya'

    Mechi nyingine Msuva alicheza dhidi ya Simba SC ni Oktoba 3, mwaka 2013 wakitoka sare ya 1-1 Amri Kiemba akianza kufunga dakika ya tatu tu, kabla ya Said Bahanuzi kuisawazishia Yanga dakika ya 65, siku ambayo Msuva alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumrudishia pigo beki Juma Said Nyosso. 
    Alicheza Mei 18, mwaka 2013 Yanga ikishinda 2-0 kwa mabao ya Didier Kavumbangu dakika ya tano na Hamisi Kiiza dakika ya 62, Oktoba 20, mwaka huo katika sare ya 3-3, wao wakitangulia kwa mabao ya Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza mawili kipindi cha kwanza kabla ya Simba SC kusawazisha kipindi cha pili kwa mabao ya Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
    Akacheza mechi ya sare ya 0-0 Oktoba 18, 2014, akacheza Machi 8, mwaka 2015 Simba SC ikishinda 1-0 kwa bao pekee la Emmanuel Okwi dakika ya 52, akacheza kwa dakika 34 Septemba 26, mwaka 2015 kabla ya kutolewa kumpisha Malimi Busungu aliyekwenda kufunga bao la pili dakika ya 79 baada ya kumsetia Amissi Tambwe kufunga la kwanza dakika ya 44 Yanga SC ikishinda 2-0.

    Kwa sasa Simon Msuva anang'ara Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco

    Akacheza Februari 20, mwaka 2016 Yanga ikishinda 2-0 kwa mabao ya Donald Ngoma dakika ya 39 na Amissi Tambwe dakika ya 72. Amecheza pia mechi zote mbili za Nani Mtani Jembe, Desemba 23, mwaka 2013 Simba SC ikishinda 3-1, mabao yake yakifungwa na Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44 kwa penalti na Awadh Juma huku la Yanga likifungwa na Emmanuel Okwi dakika ya 87.  
    Nyingine ni ya Desemba 13, mwaka 2014 Simba SC wakishinda 2-0 mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri. 
    Mechi nyingine ya watani Msuva amecheza ni ya Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi Januari 10 mwaka 2017 Simba SC ikishinda kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 tena yeye akiwa wa wafungaji wa penalti mbili za Yanga. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA: NILITAKA KUPIGWA NA MASHABIKI ETI NAIHUJUMU YANGA, LAKINI BAADAYE NIKAWAFURAHISHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top