• HABARI MPYA

    Sunday, September 02, 2018

    JKT TANZANIA YAAMKA NA KUVUNA POINTI TATU ZA KWANZA BAADA YA KUIPIGA 1-0 NDANDA FC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya JKT Tanzania imepata ushindi wa kwanza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuilaza 1-0 Ndanda FC Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, eneo la Mbweni mjini Dar es Salaam.
    Shukrani kwa mfungaji wa bao hilo pekee, Ally Bilal dakika ya 80 na sasa JKT Tanzania inayofundishwa na kocha Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ inafikisha pointi tano baada ya kucheza mechi tatu, ikipata matokeo yote, ushindi, sare na kufungwa.
    Mbao FC ndiyo wanaongoza Ligi Kuu kwa sasa wakiwa na pointi saba baada ya mechi tatu, wakifuatiwa na Azam FC wenye pointi sita za mechi mbili sawa na Simba SC. Mtibwa Sugar ina pointi sita nayo, lakini za mechi tatu.

    Mbeya City na Mwadui ndiyo pekee ambazo hadi sasa hazijavuna pointi hata moja, wakati Alliance FC na Ruvu Shooting zina pointi moja kila moja.  
    Mechi za jana, Mtibwa Sugar iliichapa Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, mabao yake yakifungwa na mshambuliaji Stahmili Mbonde dakika ya tisa na kiungo Ismail Muhesa dakika ya 42, wakati bao pekee la wageni lilifungwa na Erick Kyaruzi dakika ya 48.
    Tanzania Prisons ilishinda 2-0 dhidi ya Alliance FC Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao ya Laurian Mpalile dakika ya 20 na Ramadhani Ibata dakika ya 85, Stand United ilishinda 1-0 dhidi ya Biashara United ya Mara Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, bao pekee la mshambuliaji Mrundi, Bigirimana Blaise dakika ya 61.
    Coastal Union ililazimishwa sare ya 1-1 na KMC ya Dar es Salaam Uwanja wa Mkwakwani huko Tanga, wenyeji wakitangulia kwa bao la Hamisi Kanduru dakika ya 33 kabla ya Cliff Buyoya kuisawazishia timu ya Manispaa ya Kinondoni dakika ya 79 na Kagera Sugar imetoka sare ya 0-0 na African Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JKT TANZANIA YAAMKA NA KUVUNA POINTI TATU ZA KWANZA BAADA YA KUIPIGA 1-0 NDANDA FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top