MABINGWA watetezi, Yanga SC wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara usiku hui Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga SC leo yote yamefungwa na viungo, Mganda, Allan Jolly Okello ‘Star Boy’ dakika ya 50, mzawa Mudathir Yahya Abbas dakika ya 68 na Muivory Coast, Peodoh Pacome Zouzoua dakika ya 86.
Kwa ushindi huo, Yanga SC inafikisha pointi 41 katika mchezo wa 17 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu ikifuatiwa na watani wao, Simba SC wenye pointi 34 za mechi 15.
Kwa upande wao Tanzania Prisons baada ya kupoteza mchezo wa leo inabaki na pointi zake 13 za mechi 18 sasa nafasi ya 15 kwenye ligi ya timu 16.
Ikumbukwe mwisho wa msimu timu mbili zitashuka Daraja na mbili zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao kwa mechi mbili za nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu kutoka Ligi ya Championship katika mechi nyingine mbili za mchujo nyumbani na ugenini na mshindi wa jumla ndiye atacheza Ligi Kuu msimu ujao.



.png)
0 comments:
Post a Comment