• HABARI MPYA

    Wednesday, September 12, 2012

    ITAKUWA LIGI NZURI BILA RUSHWA

    Na Mahmoud Zubeiry

    HALI ilikuwa tete mwaka 2001, baada ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kujitoa kudhamini Ligi Kuu ya Tanzania Bara ghafla. Bingwa wa mwaka 2001, Simba SC alitoka mikono mitupu, baada ya TBL waliokuwa wakiidhamini ligi hiyo kupitia bia ya Safari Lager ‘kuimwaga’.
    Kisa nini? Kapuya huyo! Aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi, Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, ‘aliwaboa’ wadhamini hao kwa kujiamulia tu kuongeza timu katika Ligi Kuu, kinyume na makubaliano yao na Chama cha Soka Tanzania (FAT), sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    TBL wakaona ligi haina kanuni, utaratibu wala kuheshimu vipengele vya mikataba ya udhamini, wakaitema. Wengi miongoni mwa wapenzi wa soka Tanzania waliingiwa hofu juu ya mustakabali wa ligi hiyo, kwani walijua itarudi kwenye enzi zile za kucheza kwa ajili ya mapato ya milangoni tu.
    Udhamini unaongeza ladha ya ligi kwa sababu timu zinawania zawadi, mbali na kombe, zinapata vifaa vya michezo kutoka wadhamini sambamba na kiasi cha fedha za gharama kama za usafiri na kadhalika, hivyo kujitoa kwa wadhamini- maana yake ligi ingekuwa chungu kwa klabu.
    Akaibuka mkombozi, kampuni iliyokuwa mpya kabisa ya huduma za simu za mikononi Tanzania, Vodacom Tanzania na kuingia mkataba wa udhamini wa ligi hiyo na FAT, kuanzia msimu wa 2002.
    Yanga ya Dar es Salaam ilikuwa klabu ya kwanza nchini kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu chini ya udhamini wa Vodacom na leo ni miaka 10 tangu ‘Voda’ waanze kuipendezesha ligi hiyo, kila msimu wakiboresha mambo fulani fulani muhimu.
    Mkataba wa awali ulimalizika mwishoni mwa msimu na tayari makubalino ya mkataba mpya, kampuni hiyo kuendelea kuibeba ligi hiyo yamefikiwa na utasaniwa wakati wowote kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, Septemba 15, mwaka huu.   
    Huu ni msimu wa 49 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania, ambayo historia yake inaanzia mwaka 1965, wakati aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanganyika kutoka Yugoslavia, Milan Celebic, aliposhauri kuwapo kwa michuano ya kusaka klabu bingwa ya taifa, ili kujenga mazingira ya kupata wachezaji wazuri zaidi wa timu ya taifa.
    Alisema kama kutakuwa na ligi, ina maana wachezaji watakuwa wamepata mazoezi ya muda mrefu katika kujiandaa na ligi, hivyo kuwa rahisi kwake kama mwalimu wa taifa wakati huo kuona wachezaji walio fiti na kuwachukua kwenye timu ya taifa.
    FAT ilikubali ushauri huo na kuanzisha Klabu bingwa ya taifa, ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1965, ikishirikisha timu sita tu zilizoteuliwa ambazo ni TPC ya Moshi, Sunderland (sasa Simba SC), Yanga na Tumbaku ya Kurasini, Dar es Salaam, Coastal Union na Manchester United, zote za Tanga.
    Michuano hiyo ya kwanza ilifanyika katika viwanja vya Ilala (sasa Karume) na Manispaa wa Tanga, sasa Mkwakwani na tatizo kubwa lililojitokeza na viongozi wa klabu, wachezaji na hata viongozi wa FAT, ni kutozielewa vyema kanuni na sheria za mchezo, hata ikasababisha Yanga wakajitoa na ubingwa ukatolewa kwa Sunderland (Simba) walioweka historia ya kuwa mabingwa wa kwanza nchini.
    Lakini awali ya hapo, historia inasema kwamba ligi ilikuwa inachezwa Dar es Salaam pekee tangu mwaka 1929, ikishirikisha timu za Cosmopolitan, Battalion King's African Rifles (KAR), Gymkhana Club, Tanganyika Territorial Police, Tanganyika Railways, Government School na Government Services.
    Sunderland ilifanikiwa kutetea ubingwa wake msimu uliofuata, kabla ya kuutema kwa Cosmopolitan ya Dar es Salaam pia mwaka 1967.
    Lakini wakati wote huo, bado Tanzania ilikuwa haijawa mwanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), hivyo Sunderland hawakuwahi kucheza michuano ya Afrika. Cosmo ingekuwa ya kwanza kucheza Klabu Bingwa Afrika mwaka 1968 kama isingejitoa, lakini kwa kujitoa kwao, Yanga ilifungua historia ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye michuano ya Afrika mwaka 1969, baada ya kutwaa ubingwa wa Bara kwa mara ya kwanza mwaka 1968, kabla ya kuutetea mara tatu mfululizo, katika miaka ya 1969, 1970, 1971 na 1972. Baada ya hapo, Sunderland ikiwa tayari imebadili jina na kuitwa Simba kurejesha taji lake mwaka 1973.
    Simba ilishindwa kuutetea ubingwa wake msimu uliofuata, 1974 baada ya kupokonywa na Yanga katika fainali ya kihistoria iliyofanyika Uwanja wa Nyamagana, mjini Mwanza kwa kuchapwa mabao 2-1. 
    Mwaka 1975 Yanga iliutema ubingwa huo kwa Mseto SC ya Morogoro, ambayo ilipokonywa na Simba msimu uliofuata.
    Simba iliutetea ubingwa huo kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.
    Siri ya kutawala kwa Simba kwenye ligi hiyo kwa miaka yote hiyo ni kuyumba kwa Yanga baada ya kukumbwa na mgogoro mkubwa 1976, uliosababisha kukimbiwa na wachezaji wote nyota, hivyo kuanza upya kabisa kuunda timu.
    Ni ndani ya kipindi hicho Simba iliweza kulipa kisasi cha kuchapwa mabao 5-0 na Yanga mwaka 1968, wakati nayo ilipowatandika watani wao hao wa jadi 6-0 mwaka 1977. 
    Juni 1, mwaka 1968, Yanga iliigaragaza Simba 5-0, mabao yake yakitiwa kimiani na Maulid Dilunga (sasa marehemu) katika dakika za 18 kwa njia ya penalti na 43, wakati mengine yalitiwa kimiani na Salehe Zimbwe dakika ya 54 na 89, kabla ya Kitwana Manara kupachika la kuhitimisha karamu ya mabao dakika ya 86.
    Julai 19, mwaka 1977, Simba nayo ililipa kisasi kwa kuibugiza Yanga mabao 6-0, wafungaji wakiwa ni Abdallah 'King' Kibadeni aliyetikisa nyavu mara tatu katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mengine yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika za 60 na 73 na Selemani Sanga wa Yanga alijifunga dakika ya 20.
    Kufika mwaka 1981, tayari Yanga ilikuwa imara tena na kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara, ingawa msimu uliofuata iliutema kwa Pan African.
    Kuanzia mwaka 1982, mfumo wa Ligi ya Tanzania ulibadilishwa na kukawa na ligi tatu, kwanza ni igi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza visiwani Zanzibar na Ligi Kuu ya Muungano.
    Yaani baada ya kupatikana washindi wawili wa juu wa kila ligi, Bara na Visiwani, walikutana kwenye Ligi Kuu ya Muungano, kutafuta bingwa wa Tanzania na washindi wake.
    Wakati huo, bingwa wa Ligi ya Muungano alikwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika na mshindi wa pili alicheza Kombe la Washindi.
    Baadaye timu ziliongezwa na kuwa tatu kila upande katika Ligi ya Muungano.
    Mwaka 1983, Yanga ilirejesha taji hilo kwenye himaya yake, ingawa msimu uliofuata ililitema tena kwa Simba.  Kwa ujumla muongo mzima wa 1980, taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara lilikuwa la kupokonyana, kwani Simba nayo mwaka 1985 ilipokonywa taji hilo na Yanga, ambayo nayo ililitema kwa timu mpya katika Ligi Kuu msimu wa 1986, Tukuyu Stars ya Mbeya.
    Tukuyu nayo iliwarejeshea Yanga taji lao mwaka 1987, wakati mwaka 1988 Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga ilijiingiza katika orodha ya timu zilizowahi kutwaa taji hilo. Mwaka 1989, Yanga ilifunga orodha ya mabingwa wa muongo huo kwa kutwaa tena ubingwa wa Bara.
    Simba iliibuka mwaka 1990 na kutwaa ubingwa huo, ikitoka kuponea chupuchupu kushuka daraja msimu uliopita.
    Kupokonyana taji kuliendelea hata kwenye muongo wa 1990, kwani Simba iliutema ubingwa huo kwa Yanga mwaka 1991.
    Yanga iliutetea ubingwa huo mara mbili mfululizo katika miaka ya 1992 na 1993, kabla ya kupokonywa na Simba mwaka 1994. Simba ilifanikiwa kuutetea mara moja 1995.
    Mwaka 1996 ndipo Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilipozaliwa rasmi chini ya udhamini wa Bia ya Safari Lager, bia inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na ikijulikana kama Safari Lager Premier League, Yanga ndiyo iliyokuwa bingwa wake wa kwanza. Yanga iliutetea ubingwa huo kwa miaka miwili mfululizo 1997 na 1998. Mwaka 1999, Yanga ikiwa tayari imetwaa ubingwa kwa matokeo ya uwanjani, aliyekuwa Waziri wa iliyokuwa Wizara ya Kazi Maendeleo ya Vijana na Michezo, Profesa Juma Athumani Kapuya, alitengua matokeo hayo kwa kuiongezea Mtibwa Sugar pointi za mezani, hivyo kuipiku Yanga. Hatimaye Mtibwa ilipata ubingwa wa mezani.
    Mtibwa ilifanikiwa kutetea ubingwa mwaka 2000, kabla ya kupokonywa na Simba msimu uliofuata, ingawa Yanga iliibuka mwaka 2002 na kuutwaa tena ubingwa huo.
    Mwaka 2003 Simba iliyokuwa kali zaidi ilifanikiwa kuutwaa tena ubingwa huo na kuutetea mwaka 2004 kabla ya kupokonywa na Yanga 2006. Mwaka 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilifanya mabadiliko ya kalenda yake, ikitaka Ligi yake iendane na ligi za Ulaya, hivyo ikaamua kuchezesha ligi ndogo ya mpito kumpata bingwa na mwakilishi wa Kombe la Shirikisho, kabla ya Ligi Kuu kuanza rasmi Agosti.
    Simba iliibuka bingwa wa ligi hiyo, baada ya kuifunga Yanga kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4, kufuatia sare ya 1-1.
    Lakini msimu uliofuata ikiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifanikiwa kuurejesha ubingwa wake msimu wa 2008 na kutetea ubingwa hata kabla ya kucheza mechi zake tano za mwisho.
    Simba iliweka rekodi nzuri katika kumbukumbu zake, baada ya kufanikiwa kumaliza ligi na kuchukua ubingwa bila kufungwa hata mechi moja.
    Msimu uliopita, Simba walianza vizuri na kukaa kileleni kwa kipindi kirefu, lakini mechi mbili za mwisho iliporomoka na Yanga ikatwaa ubingwa katika siku ya kufunga pazia la ligi.
    Msimu uliopita, Simba wakiwa chini ya Profesa wa Kiserbia, Milovan Cirkovick walitwaa ubingwa huo kwa kishindo, wakiwafunga wapinzani wao wa jadi, Yanga mabao 5-0 katika mechi ya marudiano.
    Yanga walisingizia uongozi dhaifu chini ya Mwenyekiti, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ulisababisha majanga msimu uliopita, lakini sasa wakiwa na uongozi wa nguvu, chini ya Mwenyekiti, Milionea Yussuf Mehboob Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga, ambaye yuko njema pia, na Wajumbe ‘vibopa’ pia, akina Abdallah Bin Kleb, Mussa Katabaro na wengineo wamepania kulipa kisasa.
    Ligi itakuwa tamu. Ligi itakuwa tamu kwa sababu Azam FC, mali ya Said Salim Bakhresa imejipanga sawa sawa, baada ya kushika nafasi ya pili msimu uliopita, msimu huu inataka ubingwa.
    Unaweza kusema Ligi Kuu Bara msimu huu itakuwa mbio za farasi watatu, lakini utarajiwe upinzani pia kutoka kwa Coastal Union, Mtibwa Sugar, Toto African, Kagera Sugar, Prisons, Polisi Moro, Mgambo Shooting, African Lyon, JKT Oljoro, Ruvu Shooting na JKT Ruvu, kwani nazo zimejiandaa kikamilifu kubadilisha historia.
    Ukweli ni kwamba pamoja na ligi za jirani zetu Kenya na Uganda kurushwa na Televisheni ya kimataifa, SuperSport, lakini VPL ni ligi bora kuliko zote hizo na ndiyo maana nyota wengi wa kigeni wanavutiwa na ligi yetu yenye wachezaji hadi kutoka Magharibi na Kusini mwa Afrika.
    Dosari chache na ndogo, kama miundombinu mibovu na ufukara wa baadhi ya klabu, ni changamoto zinazoekelea kuzoeleleka, lakini ipo haja ya kupamabana nazo.
    Changamoto ambazo si vema kabisa tukazizoea ni rushwa katika katika ligi yetu, marefa wanahongwa na wachezaji wanahongwa- hili katika msimu huu mpya tupambane nalo.
    TFF iboreshe maslahi ya marefa na iwape kwa wakati, ili kukwepa kuwafanya wawe wanalipwa na klabu- kwa kufanya hivyo, kwa kiasi kikubwa itapunguza marefa kuhongwa.
    Lakini mtu anapangiwa mchezo Mbeya, anaambiwa aende bila kupewa posho wala nauli- unategemea akipewa fedha ya klabu kwa masharti ya kupendelea ataikataa huyo?
    Hili lingine la wachezaji kuhongwa, lazima TFF iliundie kitengo cha kuchunguza na iwe tayari kuchukua hatua, vinginevyo ligi yetu itabakia kuwa ya hivi hivi, ikiwa inaingia katika msimu wa 49, yaani kama ni binadamu, anaelekea uzeeni sasa, amekwishauaga ujana huyo.

    ORODHA YA MABINGWA LIGI KUU:
    1965: Sunderland (Dar es Salaam)
    1966: Sunderland (Dar es Salaam)
    1967: Cosmopolitans (Dar es Salaam)
    1968: Yanga
    1969: Yanga
    1970: Yanga
    1971: Yanga
    1972: Yanga
    1973: Simba
    1974: Yanga
    1975: Mseto SC (Morogoro)
    1976: Simba
    1977: Simba
    1978: Simba
    1979: Simba
    1980: Simba
    1981: Yanga
    1982: Pan African (Dar es Salaam)
    1983: Yanga
    1984: Simba
    1985: Yanga
    1986: Tukuyu Stars (Mbeya)
    1987: Yanga
    1988: Coastal Union (Tanga)
    1989: Yanga
    1990: Simba 
    1991: Yanga
    1992: Yanga
    1993: Yanga
    1994: Simba
    1995: Simba
    1996: Yanga
    1997: Yanga
    1998: Yanga
    1999: Mtibwa Sugar (Morogoro)
    2000: Mtibwa Sugar (Morogoro) 
    2001: Simba
    2002: Yanga
    2003: Simba
    2004: Simba
    2005: Yanga
    2006: Yanga
    2007: Simba (Ligi Ndogo)
    2008: Yanga
    2009:  Yanga 
    2010:  Simba
    2011:  Yanga
    2012:  Simba SC
    2013   ??????
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ITAKUWA LIGI NZURI BILA RUSHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top