• HABARI MPYA

  Saturday, September 08, 2018

  KILA LA HERI TAIFA STARS, WAPIGENI WAGANDA TUSAFISHE NJIA YA KWENDA CAMEROON MWAKANI

  Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
  KOCHA Mnigeria, Emmanuel Amunike leo anatarajiwa kuiongoza Tanzania kwa mara ya kwanza, itakapomenyana na wenyeji, Uganda katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Mandela, Namboole mjini Kampala.
  Amunike mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Nigeria na mshindi wa Medali ya Dhahabu ya Olimpiki mwaka 1996, alisaini mkataba wa kufundisha Stars Agosti 6, mwaka huu – hii ikiwa timu yake ya kwanza kabisa ya wakubwa ya taifa baada ya awali kuongoza timu za vijana na klabu.
  Akitumia uzoefu mdogo wa kuwa kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya kwao, Nigeria ‘Super Eagles’, Amunike anataka kuwa na mwanzo mzuri katika kibarua chake Tanzania kwa kuhakikisha anawazuia Uganda kwao. 
   
  Kambi yake ya wiki mbili kuelekea mchezo wa leo ilikumbwa na misukosuko, kufuatia kufarakana na wachezaji saba, wakiwemo sita wa klabu bingwa ya Tanzania, mabeki; Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Hassan Dilunga, Shiza Kichuya na John Bocco pamoja na kiungo wa mabingwa wa kihistoria nchini, Feisal Salum.
  Aliwafukuza kambini wachezaji hao wote chaguo la kwanza la timu kabla yake kwa kuchelewa kuingia kambini na kuchukua wachezaji ambao wengine ni wapya kabisa, akijipa matumaini anaweza kupata matokeo mazuri.
  Kikosi cha Tanzania kiliwasili Uganda Alhamisi na jana kilifanya mazoezi Uwanja wa Mandela kuelekea mchezo wa leo utakaochezeshwa na Eric Arnaud Otogo Castane atakayepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera Moussounda Montel wote wa Gabon na Issa Yaya wa Chad.
  Kwa mara ya kwanza kikosi cha Tanzania kinaingia mchezoni kikiwa na wachezaji wengi, tisa wanaocheza nje ambao ni mabeki; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na Simon Msuva Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco na washambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa BDF XI ya Botswana, Thomas Ulimwengu wa El HIlal Omduran ya Sudan na Nahodha, Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
  Wachezaji wengine kwenye kikosi cha Amunike anayesadiwa na Hemed Morocco na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Benno Kakolanya (Yanga SC), Mohammed Abdulrahman Wawesha (JKU).
  Mabeki; David Mwantika (Azam FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Paul Ngalema (Lipuli FC), Gardiel Michael (Yanga SC), Kelvin Yondan (Yanga SC), Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC), viungo; Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Frank Domayo (Azam FC), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar), Mudathir Yahya (Azam FC) na washambuliaji; Yahya Zayed (Azam FC) na Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar). 
  Amunike anasadiwa na Hemed Morocco na Mnigeriua mwenzake, Emeka Amadi.
  Taifa Stars ambayo imeshiriki AFCON moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria, ilianza vibaya mbio za Cameroon 2019 baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga aliyeondolewa.
  Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Taifa Stars. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA STARS, WAPIGENI WAGANDA TUSAFISHE NJIA YA KWENDA CAMEROON MWAKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top