• HABARI MPYA

  Thursday, September 20, 2018

  MBAO FC WAISHUGHULIKIA SIMBA SC MWANZA, WACHAPA 1-0 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU BARA

  Na Mwandishi Wetu, MWANZA
  MABINGWA watetezi, Simba SC leo wamepoteza mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
  Kwa ushindi huo, Mbao FC wanapanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wakifikisha pointi 10 baada ya kucheza mechi tano, wakiwazidi kwa pointi moja Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi tatu. 
  Simba SC wanabaki na pointi zao saba baada ya kucheza mechi nne, wakishinda mbili dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons 1-0 na Mbeya City 2-0, sare moja 0-0 na Ndanda FC na kipigo cha leo cha Mbao FC.   Bao la Mbao FC limefungwa na kiungo Said Khamis Said dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti, kufuatia mshambuliaji Pastory Athanas kuangushwa na kipa Aishi Salum Manula wakati anakwenda kufunga.
  Simba SC ilikuja juu baada ya bao hilo na kucheza kwa kushambulia mfululizo kujaribu kutafuta bao la kusawazisha, lakini sifa zimuendee kipa Hashimu Mussa aliyeokoa vizuri hatari zote.
  Kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems aliiongezea nguvu safu ya ushambuliaji ya timu hiyo kwa kumuingiza Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere akimpumzisha kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim.
  Lakini mabadiliko hayo hayakuweza kuisaidia Simba SC kupata bao zaidi tu ya kuendelea kulitia misukosuko lango la Mbao FC.
  Amri Said ‘Stam’, kocha wa Mbao FC na beki wa zamani wa Simba SC aliyeanzia ukocha timu ya vijana ya Wekundu hao wa Msimbazi, alimpumzisha Rajetsh Kotecha kipindi cha pili baada ya kazi nzuri kipindi cha kwanza na kumuingiza Evarist Mjwahuki kuongeza kasi ya mashambulizi.
  Kikosi cha Mbao FC kilikuwa; Hashim Mussa, Vincent Philipo, Amos Charles, David Mwasa, Peter Mwangosi, Ally Mussa, Said Khamis, Hussein Suleiman/Rolland Msonjo dk76, Rajesh Kotecha/Evarist Mjwahuki dk58, Pastory Athanas na Abubakar Mfaume/Hamim Abdulkarim dk90. 
  Simba SC; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Shiza Kichuya/Rashid Juma dk74, Cletus Chama, John Bocco, Emmanuel Okwi na Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Meddie Kagere dk55.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBAO FC WAISHUGHULIKIA SIMBA SC MWANZA, WACHAPA 1-0 NA KUPANDA KILELENI LIGI KUU BARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top