• HABARI MPYA

    Monday, September 03, 2018

    MANDAWA AWA WA KWANZA ANAYECHEZA NJE KURIPOTI KAMBINI TAIFA STARS YA AMUNIKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa BDF XI ya Botswana, Rashid Mandawa amekuwa mchezaji wa kwanza anayecheza nje kuripoti kambini timu ya taifa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Uganda Jumamosi wiki hii mjini Kampala, Uganda.
    Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online kwamba Mandawa aliingia kambini hoteli ya Sea Scape, Kunduchi mjini Dar es Salaam jana jioni na leo ameanza mazoezi Uwanja wa Boko Veterani.
    Msangi amesema kwamba wachezaji zaidi wanaocheza nje wanatarajiwa kuwasili leo na kesho kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.

    Rashid Mandawa amekuwa mchezaji wa kwanza anayecheza nje kuripoti kambini Taifa Stars 

    Wachezaji wengine wanaocheza nje ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo, Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida, Morocco, Farid Mussa na washambuliaji Shaaba Iddi wa CD Tenerife ya Hispania, Abdi Banda, Thomas Ulimwengu wa El HIlal ya Sudan na Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji.
    Wachezaji wengine waliopo kambini Taifa Stars ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Benno Kakolanya wa Yanga SC na Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, mabeki David Mwantika wa Azam FC, Ally Sonso, Paul Ngalema wa Lipuli FC ya Iringa, Gardiel Michael, Kelvin Yondan na Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC, Aggrey Morris, viungo ni Salum Kimenya wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Frank Domayo wa Azam FC, Salum Kihimbwa wa Mtibwa Sugar, Mudathir Yahya na washambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC na Kelvin Sabato wa Mtibwa Sugar. 
    Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike aliyesaini mkataba wa kufundisha Taifa Stars mapema Agosti, ambaye anasaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na Mzalendo, Hemed Suleiman ‘Morocco’, baada ya mechi na Uganda Septemba 8, mwaka huu mjini Kampala, atawafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza kufuzu AFCON.
    Na hiyo ni baada ya Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MANDAWA AWA WA KWANZA ANAYECHEZA NJE KURIPOTI KAMBINI TAIFA STARS YA AMUNIKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top