• HABARI MPYA

    Wednesday, September 12, 2018

    AUSSEMS ASEMA HAMJUI NIYONZIMA, SIMBA SC KUMKOSA ASANTE KWASI MECHI NA NDANDA

    Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J Aussems amesema kwamba hamjui mchezaji wa klabu hiyo Mnyarwanda Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Mbelgiji huyo ameyasema hayo leo jioni Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam wakati wa mazoezi ya mwisho wa Simba SC kabla ya safari ya Mtwara kesho asubuhi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Ndanda FC Jumamosi Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
    “Ndiyo nani Haruna? Silijui hilo jina na sijawahi kulisikia tangu nimekuja hapa,”alisema Mbelgiji huyo aliyeanza kazi Julai akimpokea Mfaransa, Pierre Lechantre baada ya kuulizwa na Waandishi wa Habari juu ya kiungo huyo kutoonekana mazoezini leo timu ikijiandaa kwa safari ya Mtwara.

    Haruna Niyonzima alijiunga na Simba SC msimu uliopita kutoka kwa mahasimu, Yanga SC

    Mbali na Niyonzima, wachezaji wengine waliokosekana mazoezini Simba SC leo ni beki Juuko Murshid, kiungo Jonas Mkude waliopewa ruhusa kushughulikia masuala yao binafsi, Asante Kwasi ambaye ni mgonjwa, Cletus Chama ambaye anatarajiwa kurejea kesho kutoka kwao Zambia alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa.
    Niyonzima yuko katika msimu wake wa pili tangu asajiliwe Simba SC kutoka kwa mahasimu, Yanga SC lakini baada ya kuandamwa na maumivu katika msimu wake wa kwanza, sasa anaonekana kuwa katika mgogoro na uongozi.
    Na hiyo ni baada ya kuchelewa kujiunga na timu kwa kambi ya maandalizi ya msimu mpya nchini Uturuki kiasi kwamba hakutambulishwa katika orodha ya wachezaji wa msimu huu wa klabu kwenye tamasha la Simba Day Agosti 8, Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam yeye pamoja na Juuko.
    Lakini wakati suala la Niyonzima likiwa bado kizungumkuti, leo Kaimu Rais wa klabu, Salum Abdallah ‘Try Again’ amesema kwamba Juuko amerejeshwa rasmi kikosini baada ya kumaliza tofauti zake na uongozi.
    Juuko pia hakwenda Uturuki kwenye kambi ya kujiandaa na msimu huu, ikielezwa alikuwa Afrika Kusini kwa majaribio lakini hata aliporejea hakuwahi kuonekana na timu.
    Hata hivyo, baada ya kucheza vizuri Jumamosi katika mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Tanzania Uwanja wa Mandela mjini Kampala, uongozi wa Simba umeamua kumpa nafasi nyingine naye ameahidi kujirekebisha.
    Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba wanatarajiwa kuondoka kesho asubuhi kwenda Mtwara kwa ajili ya mchezo wake wa tatu wa Ligi Kuu wa msimu.
    Aussems atachukua wachezaji 20 kati ya wote kwa safari ya Mtwara, ambako timu inakwenda kucheza mechi ya kwanza ya ugenini baada ya kushinda mbili za awali nyumbani dhidi ya timu za Mbeya, Tanzania Prisons 1-0 na City 2-0.
    Lakini kiungo Muzamil Yassin aliyeoa wiki iliyopita hatarajiwi kuwa miongoni mwao kwa sababu yeye ni majeruhi na leo alikuwa anafanya mazoezi mepesi peke yake.

    Patrick J. Aussems (kushoto) amesema hamjui Haruna Niyonzima

    Kwa ujumla, baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa, Ligi Kuu inarejea wikiendi hii na Ijumaa kutakuwa michezo miwili, Mwadui FC na Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga Saa 8:00 mchana na African Lyon na Coastal Union Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Saa 10:00 jioni.
    Ligi itaendelea Jumamosi Lipuli wakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Samora mjini Iringa Saa 8:00 mchana, Ndanda na Simba SC Uwanja wa Nangwanda SIjaona Mtwara Saa 10:00 jioni, Tanzania Prisons na Ruvu Shooting Saa 10:00 jioni Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbao FC na JKT Tanzania Saa 10:00 jioni Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, KMC na Singida United Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa na Biashara United na Kagera Sugar Saa 10:00 jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Musoma mkoani Mara.
    Mabingwa wa kihistoria, Yanga SC wao watateremka Uwanja wa Taifa Jumapili Saa 10:00 jioni kumenyana na Stand United, huo ukiwa mchezo wao wa pili tu baada ya ushindi wa 2-1 kwenye mechi ya kwanza dhidi ya Mtibwa Sugar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AUSSEMS ASEMA HAMJUI NIYONZIMA, SIMBA SC KUMKOSA ASANTE KWASI MECHI NA NDANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top